Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Kapt (Mst) George H. Mkuchika azindua Bodi ya ushauri ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA), 19 Mei, 2020 Ikulu Chamwino, Dodoma


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Kapt (Mst) George H. Mkuchika, leo tarehe 19 Mei, 2020 amezindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA), katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Makatibu Wakuu, Ikulu Chamwino, Dodoma.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Mheshimiwa Waziri alichukua nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kumteua Balozi Mhandisi John W.H. Kijazi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo. “Hii inaonyesha jinsi gani ambavyo Mheshimiwa Rais amelipa uzito jukumu la Usimamizi wa TGFA. Napenda kukupongeza sana wewe pamoja na Wajumbe wa Bodi kwa uteuzi wenu”. Alisisitiza Mheshimiwa Waziri

Wakala ya Ndege za Serikali ilianzishwa rasmi tarehe 17 Mei, 2002 kupitia Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya Mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2009. Wakati wa kuanzishwa kwake, Wakala hii ilikuwa chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Tarehe 23 Aprili, 2018, Serikali iliamua kuihamisha Wakala hii kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwenda Ofisi ya Rais, Ikulu kwa Tangazo la Serikali Na. 252 la tarehe 8 Juni, 2018.

Wakala ya Ndege za Serikali inatekeleza majukumu makubwa matatu (3). Kwanza, ni kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwa usalama na viwango vya hali ya juu. Pili, ni kuratibu na kusimamia ununuzi na ukodishaji wa ndege za Serikali kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Tatu, ni kuendesha na kufanya matengenezo ya ndege za Serikali kwa ufanisi unaozingatia viwango vya hali ya juu vya usalama.

“Majukumu haya ni nyeti sana, ni matarajio yangu kwamba mtailinda imani na heshima kubwa aliyowapeni Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kwamba mnaisimamia vizuri Wakala ya Ndege za Serikali ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo”. Alisisitiza Mheshimiwa Waziri

Mheshimiwa Waziri alibainisha kuwa, moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha sekta ya usafiri wa anga. “Sote tunafahamu kwamba hadi sasa Serikali imenunua ndege mpya 11. Kati ya ndege hizo, ndege nane (8) tayari zimeshapokelewa na zimeshakodishwa ATCL. Na kama alivyoeleza Mwenyekiti, ndege tatu (3) ndio zinatengenezwa na zinatarajiwa kuwasili nchini kati ya sasa na mwezi Juni, 2021. Lengo la Serikali ni kuona kwamba Tanzania inakuwa na Shirika la Ndege imara litakaloweza kushindana na mashirika mengine ya kikanda na kimataifa kwa kuanzisha na kuendesha safari nyingi za ndani ya nchi, za kikanda na za kimataifa”.

Ningependa nisistize pia kwamba suala la kuimarisha usafiri wa anga kwa kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania ni moja ya ahadi za Chama cha Mapinduzi iliyopo kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2015. Hivyo, mageuzi makubwa yaliyofanyika kataika sekta ya usafiri wa anga katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano ni utekelezaji wa Ilani hii ya CCM.

Mheshimiwa Waziri aliwaeleza Wajumbe wa Bodi hiyo kuwa, kimuundo Bodi hiyo ni chombo cha kumshauri Waziri. Hivyo ni matarajio yake kwamba mara kwa mara atapatiwa ushauri wa namna ya kuboresha ufanisi wa Wakala ya Ndege za Serikali ili kuweza kufikia malengo ya Serikali.

TGFA na ATCL zote ni taasisi za Serikali. Ni matarajio ya Serikali kuona taasisi hizi zinafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu. Ni bahati nzuri Mwenyekiti wa Bodi hii pia ndiye Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini. Anayo mamlaka makubwa pamoja na rasilimali za kutosha anazoweza kuzitumia kuhakikisha kwamba taasisi hizi mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano wenye tija.

Akimalizia hotuba yake ya uzinduzi, Mheshimiwa Waziri alisisitiza kwamba ni matarajio yake kwamba Bodi itasimamia kikamilifu Wakala ya Ndege za Serikali na kuhakikisha kwamba inakuwa na mipango na mikakati mizuri itakayoleta tija katika utekelezaji wa majukumu iliyokabidhiwa ikiendana sambamba na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma na usimamizi wa makusanyo ya fedha ya Serikali yatokanayo na ukodishwaji wa ndege kwa ATCL.

Awali kabla ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Mhandisi John W.H. Kijazi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi, alitoa maelezo mafupi kuhusiana na mikakati ya bodi hiyo katika kutekeleza majukumu yake pamoja na changamoto zinazoikabili Wakala ya Ndege za Serikali.

Na alichukua nafasi hiyo kwa niaba ya Wajumbe wa Bodi kumshukuru Mheshimwa Rais, Dkt. John P. Magufuli kwa kuwa na imani nao na kuwateua kuitumikia bodi hiyo na Serikali kwa Ujumla na kuahidi kuwa watatekeleza majukumu yao kiuweledi na kikamilifu.

Baada ya Mheshimiwa Waziri kuizindua bodi hiyo, wajumbe waliendelea na kikao ambacho kilikuwa ni cha kwanza kufanyika baada ya kuzinduliwa kwake.