Habari
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka atembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Balozi Dk. Mosses Kusiluka amewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yalivyokuwa na mabadiliko makubwa ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana.
Amesema maonesho hayo yamekuwa na mabadiliko makubwa kutokana na kupiga hatua katika ukuaji wa matumizi ya teknolojia.
Aliyasema hayo tarehe 04 Julai, 2024, wakati alipoyatembelea maonesho hayo na kusema kuwa mwaka huu maonesho hayo yamepiga hatua kubwa na kuwa ya kiteknolojia zaidi.
"Watanzania wenyewe tumebadilika, tumechangamka kuwa wabunifu na kukumbatia teknolojia mpya naona fahari kuwa Mtanzania,"alisema na kuongeza.
"Hata teknolojia za nje zinakuja kwa sababu wanajua kuna watu watashirikiana nao, inawezekana ukaja bila wazo ukapata wazo la kibiashara,” alisema.
Aidha alisema kwa mwaka huu washiriki wamekuwa wengi zaidi ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana ambapo ushiriki wa wenyeji ni zaidi ya 3200 na wageni wakiwa zaidi ya wafanyabiashara 400.
Mhe. Balozi Dkt.Kusiluka alisema katika maonesho hayo kuna mabanda ya nchi mbalimbali hii ikidhihirisha kuwa maonesho hayo ya kimataifa yanazidi kukua ikionesha nchi inazidi kukua inaaminika.
"Kuona ni kuamini, sote tunafahamu ufunguzi wa maonesho haya umefanyika na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi alikua mgeni rasmi kwenye ufunguzi akiambatana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, nawakaribisha Watanzania wote waje kuona maonesho haya" alisema.