Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

NDOTO YA RAIS DKT. SAMIA NI KUWA NA MASHIRIKA YENYE UFANISI - BALOZI DKT. KUSILUKA


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka amesema kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inakuwa na mashirika yenye ufanisi mkubwa na wa viwango vya kimataifa.

 

Hivyo, amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi na Mashirika ya Umma kuhakikisha wanatekeleza kwa ukamilifu maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. Samia.

 

Katibu Mkuu Kiongozi ametoa kauli hiyo leo Agosti 30, 2024 jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika jijini humo kuanzia Agosti 27 hadi 30, 2024.

 

Aidha, alieleza kuwa Serikali inayachukua maazimio yote yaliyotolewa katika kikao kazi hicho na kuahidi kuwa yatafanyiwa kazi kwa ukamilifu ili kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuwa na taasisi na mashirika ya umma yenye ufanisi na tija.

 

Amewataka viongozi wa taasisi na mashirika ya umma kujenga utamaduni wa kujifunza mbinu na  mikakati mipya kutoka mashirika yaliofanikiwa na kuhimiza juu ya matumizi bora ya rasilimali za taasisi na mashirika ya umma kwa manufaa ya nchi.