Habari
TUMIENI UZOEFU WENU KUHARAKISHA MADADILIKO - BALOZI DKT. KUSILUKA
Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi wamehimizwa kutumia taaluma, uzoefu na ujuzi tofauti waliokuwa nao kuharakisha mabadiliko ya kimfumo yanayoendelea ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili, 23, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka alipokutana na Mabalozi hao katika warsha ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayofanyika Kibaha mkoani Pwani.
"Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mmebarikiwa kuwa na watu wenye taaluma tofauti na wenye historia ya sekta tofauti, tumieni fursa yenu hii kumsadia Mwanadiplomasia namba moja, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewarahisishia kazi yenu kwa kuitekeleza diplomasia kivitendo", Balozi Kusiluka alisema.
Amesema Serikali inazitambua changamoto wanazokabiliana nazo na inazifanyia kazi lakini kutokana na Wizara kuwa na watu wenye uzoefu wa kutoka sekta tofauti, wakishirikiana wanaweza kuzitatua na kuifikisha nchi katika hatua nzuri.
Balozi Dkt. Kusiluka alimalizia kwa kuwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwaahidi kuwa Serikali itapokea mawazo yote mazuri na ya kibunifu na kuyafanyia kazi.