Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Serikali ya Tanzania yapongezwa kwa vita dhidi ya rushwa


Washirika wa Maendeleo wa Tanzania wakiwemo baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na mashirika ya Kimataifa wameelezea kuridhishwa kwao na juhudi za Serikali ya awamu ya Nne ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Jakaya Kikwete, katika mapambano dhidi ya Rushwa nchini.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue mara baada ya kukutana na baadhi ya Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ikiwemo Benki ya Afrika,Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa(International Monetary Fund) Ikulu jijini Dar es Salaam leo jioni.

Yaliyojitokeza katika mkutano huu ni wao kutambua juhudi za serikali yetu kuimarisha vita dhidi ya rushwa kwa kuimarisha taasisi zinazohusika moja kwa moja kwa kuziongezea bajeti na kuajiri wafanyakazi wenye uwezo na ujuzi wa kutenda kazi kwa weledi.Ofisi hizi ni pamoja na TAKUKURU, ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mahakama, Sekretarieti ya Maadili ya Umma na Polisi, alisema Balozi Sefue.

Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuwa washirika hao wa maendeleo wamefurahi kutambua kwamba Serikali imeongeza idadi ya watumishi wa umma wanaofanya kazi katika taasisi zinazohusika na vita vya rushwa nchini na kuboresha utendaji baada ya kupata mafunzo na kwamba miundombinu ya taasisi hizi ikwemo majengo ya ofisi na vitendea kazi vimeimarishwa.

Balozi Sefue aliongeza kusema kuwa washirika hao wa maendeleo wamekuwa wawezeshaji wakuu wa taasisi zinazopambana na rushwa nchini kwa kuzichangia kwa fedha na kugharamia mafunzo ya baadhi ya watumishi wa taasisi hizo na kwamba katika mkutano wa leo wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika vita dhidi ya rushwa kwa kuisaidia Serikali kuimarisha mifumo, sheria, taratibu na kutoa mafunzo kwa watumishi.

Baadhi ya Washirika wa Maendeleo waliohudhuria mkutano wa Katibu Mkuu kiongozi ni pamoja na wawakilishi kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), Balozi wa Uingereza nchini, Balozi wa Canada,Balozi wa Norway,Balozi wa Finland, Balozi wa Denmark,Balozi wa Ujerumani, Balozi wa Ireland, Balozi wa Sweden, Mwakilishi wa Ubalozi wa Japan, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mwakilishi wa Benki ya Dunia na Mwakilishi wa Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF). Januari 23, 2014