Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na kuwa Katibu Mkuu Kiongozi – 27/02/2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Februari, 2021 amemuapisha Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa imefanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwake, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha kwake kwa kumteua katika wadhifa huo mkubwa na ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa juhudi na maarifa, kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, mila na desturi za wadhifa huo.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amewaomba Watanzania kumuombea ili atekeleze majukumu yake kama yalivyo matarajio ya Mhe. Rais Magufuli ambaye amejipambanua kwa kupigania maslahi ya nchi, kuwapigania Watanzania hasa wanyonge na kuimarisha mawasiliano Serikalini ili kutoa huduma bora kwa wananchi.