Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Watumishi wa Umma wametakiwa kuzingatia maadili


Watumishi wa Umma nchini wametakiwa kuwa wabunifu na kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili utendaji wao uweze kuwa na tija kwa Taifa. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema hayo wakati alipotembelea Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma  na kukutana na  Menejimenti  pamoja na Watumishi wa ofisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya utaratibu aliojiwekea  wa kutembelea Wizara na Taasisi za Umma ili kujionea shughuli mbalimbali za Serikali zinavyotekelezwa.

“Naomba niweke wazi kuwa Utumishi wa Umma hivi sasa unahitaji Watumishi wenye ujuzi, weledi na maadili mema na si vinginevyo, hivyo ni vyema kila mtumishi akatimiza wajibu wake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma” alisisitiza Balozi Ombeni.                                                                           

Balozi Sefue pamoja na Ujumbe wake waliweza kupata maelezo ya kina ya namna majukumu ya mchakato wa ajira yanavyotekelezwa na ofisi hiyo. Aidha, aliweza pia kutembelea baadhi ya maeneo ikiwemo eneo la masjala na maeneo mengine ya ofisi na kupata maelezo kuanzia hatua za awali barua zinavyopokelewa hadi waombaji wa fursa za ajira wanapoitwa kwenye usaili.

Akijibu maswali ya Watumishi pamoja na Waandishi wa Habari alisema Serikali ilifanya uamuzi wa busara sana kwa kuanzisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwani imeweza kusaidia kupatikana kwa watumishi wenye sifa stahili za kufanya kazi katika Utumishi wa Umma.

Alifafanua kuwa hivi sasa ili mtu aweze kuingia Seriklini ni lazima apitie chombo hicho kwa mujibu wa sheria maana kinachotakiwa ni mwombaji kukidhi vigezo vya nafasi iliyotangazwa na kuachana na ile dhana iliyokuwa imejengeka kwa baadhi ya watu kuwa ili upate kazi Serikalini ni lazima uwe unamfahamu mtu na sio unajua nini.

Katibu Mkuu Kiongozi pia aligusia kuhusu suala la waombaji kughushi baadhi ya taarifa ikiwemo vyeti vya kitaaluma pindi wanapowasilisha maombi ya kazi Sekretarieti ya Ajira na kusema kuwa tatizo hilo sio la Tanzania peke yake bali hata nchi zilizoendelea lipo. 

“Msije mkasema ni Tanzania peke yake ndio watu wanaghushi vyeti, maana hata nchi nyingine tatizo hilo lipo, ndio maana Sekretarieti ya Ajira kwa kushirikiana na Taasisi nyingine ikiwemo Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi (VETA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) wameweza kubaini jumla ya vyeti vya kughushi 699”.

Pia aliwataka waombaji wa fursa za ajira nchini kuachana na tabia ya kughushi vyeti  maana hivi sasa Sekretarieti ya Ajira pamoja na mamlaka zingine ikiwemo VETA, RITA na NECTA  ziko katika mazungumzo ya kuona namna ya kuwachukulia hatua za kisheria wale waliokwisha bainika kughushi taarifa pamoja na vyeti katika kuwasilisha maombi ya kazi. 

Mwisho alimaliza kwa kusema kuwa amepokea changamoto ambazo Sekretarieti ya Ajira inakabiliana na nazo ikiwemo suala la ufinyu wa bajeti hivyo ataona namna atakavyoweza kulishughulikia ili chombo hicho kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.