Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Ofisi ya Taifa ya Usalama Serikalini wakabidhi Kitabu cha Mwongozo wa Kanuni za Usalama Serikalini kwa Katibu Mkuu Kiongozi – Dodoma 10 Januari, 2020


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John W. H. Kijazi, leo tarehe 10 Januari, 2020 amekabidhiwa Kitabu cha Mwongozo wa Kanuni za Usalama Serikalini, na Bwana Mululi M. Mahendeka ambaye ni Afisa Usalama wa Serikali. Muongozo huo umeandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Usalama Serikalini, makabidhiano hayo yamefanyika ofisini kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu ya Chamwino, Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma.

Akikabidhi kitabu hicho, Bw. Mahendeka alisema zoezi la kukabidhi nakala za kitabu hicho kwa watendaji wakuu wa serikali litafanyika kwenye ofisi zote za serikali zilizopo Makao Makuu ya Serikali Mkoani Dodoma pamoja na mikoa mingine yote nchini. Aidha, alibainisha kuwa kitabu hiki kilichopigwa chapa na Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ni toleo la mwaka 1999 ambalo limefanyiwa maboresho mwaka jana 2019 ili kuendana na mabadiliko mbalimbali yaliyopo katika utendaji kazi Serikalini na utekelezaji wa kanuni za usalama Serikalini.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi alitoa maelekezo kwa Ofisi ya Usalama Serikalini, kuongeza nguvu katika kutoa elimu na mafunzo ya mara kwa mara kuhusu kanuni za usalama Serikalini kwa watumishi wa Umma wa ngazi zote, ili waweze kuzielewa na kuzifuata kikamilifu katika utendaji wao wa kazi wa kila siku kwa faida ya Serikali na Taifa kwa ujumla.