Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bibi Bella Bird amuaga rasmi Katibu Mkuu Kiongozi 13 Januari, 2020


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi, John W. H. Kijazi, leo tarehe 13 Januari, 2020 amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bibi Bella Bird ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam kwa kikao kifupi ambapo pamoja na mambo mengine, Bibi Bird alichukua nafasi hiyo kumuaga rasmi Katibu Mkuu Kiongozi baada ya kumaliza muda wake kama Mkurugenzi Mkazi wa Benki hiyo kwa nchi za Tanzania, Malawi, Zambia, Msumbiji na Somalia.

Katika kikao hicho Bibi Bird alibainisha kuwa muda wake wa kuitumikia Benki hiyo nchini uliisha Juni, 2019 ila aliongezewa muda wa ziada na sasa anatarajia kuondoka rasmi tarehe 16 Januari, 2020 kwenda nchini Zambia na Msumbiji kwa ajili ya kuaga rasmi.

Mkurugenzi huyo ameelezea furaha yake kutokana na miradi mbalimbali inayoendelea nchini chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, na pia alimshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa ushirikiano wake hasa kutafuta majibu pale kunapokuwa na mkwamo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini. Aliahidi kuwa ataendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania akiwa makao makuu ya Benki hiyo jijini Washington DC, nchini Marekani, vilevile, ameahidi kuwa atamkabidhi ofisi Mkurugenzi mpya ambaye ana imani kuwa ataendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania.