Habari
Leo tarehe 14 Machi, 2017, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. John W.H. Kijazi, amekutana kwa mazungumzo na wadau wa sukari nchini.
KATIBU MKUU
KIONGOZI AKUTANA NA WADAU WA SUKARI NCHINI
Leo tarehe 14 Machi, 2017, Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. John W.H. Kijazi, amekutana kwa mazungumzo na wadau
wa sukari nchini. Wadau hao ni kutoka katika Bodi ya Sukari Tanzania; Chama cha
Wazalisha Sukari Tanzania; na Chama cha Wakulima wa Miwa Tanzania.
Wengine walioshiriki ni kutoka Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu); Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Kilimo);
Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; na Kituo cha Uwekezaji nchini.
Pamoja na mambo mengine, Kikao
kimejadili maendeleo ya sekta ya sukari nchini na kutathmini hali ya
upatikanaji wa sukari kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwishoni mwa mwezi Februari
2017. Aidha, wadau wamejadili suala la utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa
wazalishaji wa sukari kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la
ndani.
Katibu Mkuu Kiongozi amewataka wadau
wote, hususan Wazalishaji wa Sukari na Wakulima wa Miwa kushirikiana katika
kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa sukari ya kutosha kwa
matumizi ya ndani.
Aidha, amemtaka Katibu Mkuu
anayeshughulikia Kilimo kukutana na wadau hao kuzungumzia changamoto mbalimbali
zinazowakabili na kupata maoni yao ya namna ya kuzipatia ufumbuzi.