Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KILA MMOJA ANAWAJIBU WA KUJENGA UADILIFU WA KUTOKUTOA WALA KUPOKEA RUSHWA - KATIBU MKUU KIONGOZI. 04-03-2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, amesema kujenga uadilifu kwa kila mtu katika nchi yake, ni kukataa kutoa au kupokea rushwa.

Balozi Sefue aliyasema hayo wakati akifungua Warsha ya kujadili Rasimu ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi, Watumishi wa Umma na wa Sekta binafsi iliyoandaliwa na Tume ya Maadili na kufanyika katika ukumbi wa Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam leo tarehe 4 Machi, 2015.

Wazo la Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi, watumishi wa umma na wa sekta binafsi ni mwanzo mzuri wa kampeni ya nchi nzima ya kupinga vitendo vya rushwa, pamoja na sheria kali na adhabu zilizopo, lakini iwe ni dhamira ya kila mmoja kufuata maadili na kujenga utamaduni wa kutotoa au kupokea rushwa, alisema.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuwa Ahadi hizo zitumike kama muongozo na kuzingatiwa na viongozi, watumishi wa umma na wale wa sekta ya binafsi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hivyo kuchangia katika juhudi za kupambana na rushwa nchini.

Balozi Sefue alibainisha kuwa lengo la 3.2 la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, inayohusu Uongozi bora na Utawala wa Sheria, inakusudia Tanzania kuwa jamii yenye; maadili mema, utamaduni, uadilifu, kuheshimu utawala wa sheria na kutokuwepo kwa rushwa na maovu.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Maadili, Jaji Mstaafu, Salome Kaganda, alisema Rasimu ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi, Watumishi wa Umma na wa Sekta binafsi ni juhudi za kuunga mkono jitihada zilizopo za kukuza uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika kuimarisha utawala bora nchini.

Jaji Kaganda alisema kuwa, waliokuwa wakiangaliwa ni watumishi wa umma tu, lakini sasa watahusishwa pia watumishi wa sekta binafsi, wanasiasa na wafanyabiashara katika kujenga utawala bora nchini.