Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KIKAO CHA MAKATIBU WAKUU WA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA (SJMT) NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR (SMZ) CHA KUJADILI MASUALA YA MUUNGANO KILICHOFANYIKA IKULU - DAR ES SALAAM TAREHE 22 SEPTEMBA, 2023


Tarehe 22 Septemba, 2023, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka akiwa na Mwenyekiti Mwenza Mhandisi Zena A. Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi (SMZ), ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ kilichojadili masuala ya Muungano. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Jakaya M. Kikwete uliopo Ikulu, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano wa Mwaka 2019, Vikao vya Kamati ya Pamoja vinafanyika katika ngazi tatu ambazo ni: Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano; Kikao cha Mawaziri wa SJMT na SMZ; na Kikao cha Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ. Vikao vyote huratibiwa na Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambayo ina wajumbe nane (8), wanne (4) kutoka SJMT na wajumbe wanne (4) kutoka SMZ.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Makatibu wa Wakuu wote wa SJMT na SMZ pamoja na Naibu Wanasheria Wakuu wa Serikali wa SJMT na SMZ ambao ndio wajumbe wa kikao hicho.

Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ kilichofanyika Dodoma tarehe 6 Desemba, 2022 kilitoa maagizo ya kufanyia kazi hoja nne (4) zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi. Hivyo, kikao cha Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ kilichofanyika leo kimepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka amewaasa Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ kuendeleza utaratibu uliowekwa na Serikali zote mbili wa kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara, Idara na Taasisi zisizo za Muungano za pande mbili kwani ushirikiano uliopo umesaidia kupunguza changamoto za Muungano na kuimarisha utekelezaji. Naye Mwenyekiti Mwenza, Mhandisi Zena A. Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi (SMZ) amepongeza namna ambavyo pande mbili zimeimarisha ushirikiano na kuwaasa Makatibu Wakuu wa pande mbili za Muungano waendelee kuimarisha ushirikiano uliopo.

Baada ya kikao cha Makatibu Wakuu wa SJMT na SMZ kitafuata kikao cha Mawaziri wa SJMT na SMZ na baadaye Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambacho Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.