Habari
Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara, Balozi Mha. John W. H. Kijazi aongoza Mkutano wa 32 wa Kamati ya Utendaji ya Baraza hilo jijini Dar es Salaam.
Leo tarehe 23 Septemba, 2016, Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Balozi Mha. John W. H. Kijazi ameongoza Mkutano wa Kamati Tendaji wa Baraza hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Baraza zilizopo katika Jengo la TANHOUSE, barabara ya Ali Hassan Mwinyi Dar es Salaam.
Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika tangu Wajumbe wa Baraza hilo wapatao
40 (20 kutoka sekta binafsi na 20 kutoka sekta ya umma) wateuliwe na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli mapema
mwaka huu.
Katika majadiliano hayo, wawakilishi wa sekta binafsi wakiongozwa na
Mwenyekiti Mwenza, Dk. Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP walisisitiza
umuhimu wa mahusiano ya karibu baina ya Serikali na sekta hiyo na hivyo
kupongeza uamuzi wa kufanyika kwa Mkutano huo. Aidha, walipongeza hatua
mbalimbali za Serikali zenye lengo la kuweka mazingira mazuri zaidi kwa
biashara na uwekezaji nchini, hususan uwekezaji wa ndani. Vilevile waliahidi
kuendelea kuunga mkono azma ya Serikali ya kujenga nchi ya uchumi wa viwanda, suala
ambalo wamependekeza liwe ni mada kuu katika Mkutano ujao wa Baraza hilo.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji, Balozi
Mha. John W. H. Kijazi aliwashukuru Wajumbe kutoka sekta binafsi kwa kuteuliwa
kuwawakilisha wafanyabiashara wenzao katika Baraza hilo. Aidha, aliwahakikishia
kuwa Serikali inaheshimu na itaendelea kudumisha mahusiano chanya baina yake na
sekta binafsi, kwani inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika ujenzi wa taifa.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kutumia jukwaa hilo kuweka mikakati ya pamoja
na kuendeleza sekta ya biashara na kukabiliana na changamoto zinazoikabili.
Baraza la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa
mwaka 2001 likiwa na jukwaa mahsusi la majadiliano baina ya sekta binafsi na
sekta ya umma. Vilevile, Baraza liliundwa kwa lengo la kuhamasisha uboreshaji
wa mazingira ya biashara na uwekezaji, wa ndani na nje; pamoja na suala zima la
maendeleo ya sekta binafsi ambayo ni mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi na
maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kamati ya Utendaji, ni sehemu muhimu ya Baraza hilo yenye jukumu la kusimamia utendaji wa kila siku wa Baraza. Kamata hukutana mara nne kwa mwaka kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwenye mikutano iliyotangulia, ikiwemo Mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara.