Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa wamemtembelea Rais Mstaafu wa Awamu ya nne (4) Mhe. Jakaya M. Kikwete Ofisini kwake, Masaki Dar Es Salaam.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein A. Kattanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya uendeshaji wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), akiambatana na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi  (Commandant), Meja Jenerali Ibrahim Mhona, leo tarehe 05 Septemba, 2022 wamefanya ziara ya kumtembelea Rais mstaafu wa awamu 4 Mhe. Jakaya M. Kikwete ofisini kwake Masaki jijini Dar es Salaam. Lengo la ziara hiyo ni kuwasilisha mwaliko rasmi kwa Rais Mstaafu Mhe. Kikwete na kumkaribisha katika kilele cha maadhimisho ya miaka kumi (10) tokea kuanzishwa kwa chuo hicho. Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa fupi kuhusu maadhimisho ya sherehe ya miaka kumi (10) ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (National Defence College) zinazotegemewa kufanyika tarehe 8 Septemba, 2022.

Mkuu wa chuo hicho (Commandant), Meja Jenerali Ibrahim Mhona alielezea kuwa shughuli mbalimbali zinazotegemea kufanyika katika wiki ya kuelekea kilele cha maadhimisho hayo ni pamoja na upandaji miti eneo la chuo hususani kwenye kingo za mto Tegeta ili kuzuia mmomomyoko wa udongo, kufanya usafi katika eneo la Coco Beach, kutembelea hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Kutembelea vituo vya kulelea watoto yatima vya NEW LIFE ORPHAN Home kilochopo Tegeta Basi Haya na MOTHER OF MERCY kilichopo Madale. Vilevile ilielezwa kuwa tarehe 7 Septemba 2022, kutakuwa na kusanyiko (Convocation) ambapo washiriki watakuwa ni wahitimu wa chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012.

Meja Jenerali Mhona alieleza pia kuwa, kilele cha sherehe za maadhimisho hayo kitakuwa tarehe 8 Septemba, 2022 na mgeni rasmi atakuwa Mhe. Samia Hassan Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Aidha, kama sehemu ya maadhimisho hayo, kutakuwa na Kongamano (Symposium) ambapo viongozi na wadau mbalimbali wamealikwa. Kongamano hilo linaenda sambamba na kauli mbiu “Uhuru wa Tanzania, Ujenzi wa Taifa, Usalama na Maendeleo”.  Mhe. Kikwete anatarajiwa kuwa mzungumzaji Mkuu (Key note speaker).