Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga atembelea maonyesho ya wiki ya Sheria - Dodoma


Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga leo tarehe 26/01/2022 ametembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria nchini yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma ambapo ameipongeza Mahakama kwa uboreshaji wa huduma huku akishauri kuhusisha wanafunzi katika matukio mbalimbali ili kuwapa hamasa ya kuipenda fani ya sheria.

Akizungumza mara baada ya kukagua mabanda kadhaa yaliyopo katika Maonesho hayo tarehe 26 Januari, 2022, Balozi Kattanga alisema kuwa amefurahi kuwa Mahakama imepiga hatua katika uboreshaji wa huduma mbalimbali zinazotolewa.

“Nina furaha kuwa katika kipindi cha takribani miaka mitatu (3) niliyotoka mahakamani naona kuna mabadiliko makubwa ambayo yametokea hususani upande wa mifumo ya TEHAMA. Hata hivyo naomba utaratibu wa kuwahusisha Wanafunzi wa shule mbalimbali uendelee ili kuwajenga Watoto kuipenda fani ya sheria bado mapema,” alisema Balozi Kattanga.

Aidha; Katibu Mkuu Kiongozi ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mhimili wa Mahakama ili kuuwezesha Mhimili huo wa Mahakama kuendelea kutoa haki kwa wananchi.

Balozi Kattanga alipata pia fursa ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma na vilevile kukagua Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayojengwa katika eneo la Tambuka reli jijini Dodoma ambapo pia ameonyesha kufurahishwa na ubora wa jengo la 'IJC' Dodoma na hatua kubwa iliyofikiwa ya mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Mahakama.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemshukuru Katibu Mkuu Kiongozi kwa kutenga muda wake na kuamua kuja kutembelea maonesho hayo, kutembelea jengo la 'IJC' na kukagua mradi wa ujenzi wa Makao makuu ya Mahakama.

"Nikiri wazi kuwa nimefurahishwa na ujio wako Mhe. Balozi Kattanga, na tunashukuru kwa ushirikiano ambao Serikali inaendelea kutupa, kutuwezesha kutimiza ili malengo yetu, tunaahidi kuendelea kuboresha huduma na kuendeleza mazuri yote uliyoyaacha ukiwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama," alisema Prof. Ole Gabriel.