Habari
Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses M. Kusiluka aongoza kikao kazi cha Makatibu Wakuu - 11/01/2023
Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Mpogole Kusiluka leo tarehe 11/01/2023 kwa mara ya kwanza ameongoza kikao kazi cha Makatibu Wakuu na Wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na wale wa sekta ya Nishati.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 03/01/2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimteua Dkt. Moses Kusiluka kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya Balozi Hussein A. Kattanga ambaye ameteuliwa na Mhe. Rais kuwa Balozi wa Tanzania mjini New York, nchini Marekani na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa.
Katika kikao hicho ambacho kilifanyika katika ukumbi wa Mikutano na Shughuli mbalimbali wa Jakaya Kikwete uliopo Ikulu jijini Dar es Salaam, waraka wa “Tathmini ya hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022/23 na mwelekeo hadi Juni 2023” uliowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ulijadiliwa, pamoja na nyaraka nyingine za sekta ya Fedha,Uwekezaji, Viwanda na Nishati.
Vilevile katika kikao hicho Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Bw. Mululi Majula Mahendeka pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, walipata nafasi ya kujitambulisha kwa wajumbe wa kikao hicho kufuatia uteuzi wao hivi karibuni kushika nafasi hizo.