Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE AWAASA MAKATIBU MAHSUSI KUZINGATIA KWA DHATI MAADILI YA KAZI YAO, CHIMWAGA DODOMA, 29 MEI, 2015
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 29 Mei, 2015 amewaasa Makatibu Mahsusi katika sekta ya umma na sekta binafsi kuzingatia kwa dhati maadili ya kazi yao. Balozi Sefue aliyasema hayo alipokuwa akifungua Mkutano wa Tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) katika Ukumbi wa Mikutano wa Chimwaga, Dodoma.
Balozi Sefue alisisitiza kuwa ni muhimu wakatambua majukumu yao na wajibu wao kwa taasisi wanazofanyia kazi, kwa viongozi wao na hatimaye kwa taifa, kwa ujumla. Na akawatahadharisha kuwa wao ndio sura na taswira ya taasisi wanazofanyia kazi na ya wakuu wao wa kazi na kwamba ni jambo la kawaida kwa binadamu kupata taswira ya mtu au ofisi kwa kile anachokiona mwanzo.
Vilevile, amewataka wasitetereke katika jukumu lao la kutunza siri za ofisi na kwamba uadilifu na uaminifu ndio njia pekee ya kuaminiwa na wakuu wao wa kazi. Balozi Sefue amewataka pia wajiendeleze kielimu kwani ipo mifano ya waliofanya hivyo hata wakafikia ngazi ya watendaji waandamizi.
Balozi Sefue alielezea pia kukasirishwa kwake na waajiri na wakuu wa kazi wanaowanyanyasa Makatibu Mahsusi na akaagiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuangalia uwezekano wa kuwa na ‘hotline’ ya kuripoti vitendo vya aina hiyo na kuchukua hatua kali za kinidhamu.
Mkutano wa Tano wa TASPEA ulianza tarehe 28 Mei, 2015 na unatarajiwa kumalizika tarehe 30 Mei, 2015.
NB: Tembelea tovuti hii ili kusoma hotuba nzima ya Katibu Mkuu Kiongozi.