Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE ATEMBELEA MABANDA YA MAONYESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM. 22 JUNI, 2015.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 22 Juni, 2015 ametembelea mabanda ya maonyesho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

 

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwakaa huu yamebeba kaulimbiu isemayo: Utumishi wa Umma Katika Bara la Afrika ni Chachu ya Kuwawezesha Wanawake, Kuongeza Ubunifu na Kuboresha Utoaji Huduma kwa Umma”.


Katika maelezo yake ya utangulizi Balozi Sefue ameonyesha kufurahi kwake kwa namna jinsi maonyesho ya mwaka huu yalivyofana. Taasisi karibu zote zimejitahidi kuonyesha shughuli zao kwa ubunifu na umahiri mkubwa.

 

Aidha, alisema pia kwamba watumishi wengi wa umma wanajitahidi sana kutekeleza wajibu wao ingawa wapo watumishi wachache wanaokiuka taratibu na maadili ya utumishi wa umma. Hivyo, aliwaomba watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na ubunifu mkubwa ili kuweza kukabiliana na changamto za wakati.

 

 Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi aliwataadharisha watumishi wote kuacha ushabiki wa kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu,  badala yake wachape kazi bila upendeleo. Aidha, aliwaeleza kuwa watumishi wanaotaka kuingia katika masuala ya siasa wazingatie taratibu na mwongozo uliowekwa na Serikali.

Katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fulsa ya kuzindua Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma. Alisisitiza kuwa Bodi iutangaze mkataba huo na kutekeleza mihadi (commitments) na viashiria (indicators) vilivyomo kwenye mkataba husika.

 

Mwisho Balozi Sefue alitoa wito kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kwenda kutembelea mabanda na kupata taarifa na huduma mbalimbali.

 

Balozi Sefue alitembelea jumla ya mabanda ishirini (20) ambayo ni: MOI, Bunge la Tanzania, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, TCRA, PPF, GEPF, SSRA, OSHA, NHIF, TFDA, eGA, MKURABITA, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Ofisi ya Waziri Mkuu, TRA, NMB, Wakala wa Vipimo, NAO, Ofisi ya Rais – Utumishi na TaGLA.