Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, ASHIRIKI UFUNGUZI RASMI WA KITUO CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU NA NYARAKA DODOMA, 18 MACHI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 18 Machi, 2015 amejumuika na viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama, Taasisi na Mashirika ya Umma na Wananchi waliofika kwenye Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka kilichopo eneo la Kisasa mjini Dodoma kwa ajili ya uzinduzi rasmi. Kituo hicho kimejengwa chini ya Programu ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma (PSRP) kwa fedha za Serikali pamoja na Washirika wa Maendeleo ambao ni Serikali ya Uingereza (DFID), Canada (CIDA) na Benki ya Dunia.

Katika hotuba ya ufunguzi, Rais, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alielezea furaha yake kutokana na kazi nzuri ya ujenzi wa kituo hicho cha kisasa kitakachosaidia katika kupokea, kufanya tathmini na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka zenye umuhimu wa muda mrefu na akawasihi Washirika wa Maendeleo kuendelea kukiimarisha kituo hicho ili kiweze kutoa huduma inayotarajiwa. Mhe. Rais akahitimisha hotuba yake kwa kuiagiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuangalia uwezekano wa kuanzisha Maktaba za Viongozi wa Kitaifa hasa Marais Wastaafu ili kuhifadhi vyema historia ya nchi.

Sherehe hizo zilipambwa na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya ngoma na bendi za Jeshi la Polisi na Magereza.