Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE, AHITIMISHA ZIARA YAKE MIKOA YA KANDA YA KASKAZINI.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 19/9/2014 amemaliza ziara yake mikoa ya Kanda ya Kaskazini mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. Awali, alianza ziara yake hiyo tarehe 15/9/2014 katika mji wa Kibaha mkoani wa Pwani na kufuatia mikoa ya Tanga, Manyara na Arusha.

Akihitimisha ziara yake, alianza ratiba yake kwa kuongoza Mkutano wa Wadau wa uwekezaji katika Mkoa wa Kilimanjaro. Miongoni mwa wadau muhimu waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Eliakim Maswi na wawakilishi kutoka Tume ya Mipango, Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, Kilimo, Chakula na Ushirika, Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akimkaribisha Katibu Mkuu Kiongozi kuongoza Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama alisema kuwa, lengo la mkutano huo ni kupata mawazo, maoni na michango ya wadau kwa ajili ya kuboresha maandiko ya miradi iliyobuniwa na mkoa. Miradi hiyo ni; ujenzi wa mnara wa kitalii wenye urefu wa mita 600, ujenzi wa soko la mazao ya nafaka, maua na mbogamboga na ujenzi wa mji wa kisasa wa Viwanda na Biashara.

Kutokana na michango na maoni mbalimbali, Katibu Mkuu Kiongozi aliungana na wajumbe wa mkutano kuupongeza uongozi wa mkoa katika jitihada walizofanya za kubuni miradi hiyo. Aliushauri kuwa, uongozi wa mkoa uzingatie mambo yafuatayo:-

  1. Uwashirikishe  wadau wote muhimu ikiwa ni pamoja na sekta binafsi.
  2. Uandae mpango kazi wa miradi utakaoweka mfumo wa namna miradi itakavyoendeshwa na kusimamiwa.
  3. Uwasiliane na waendeshaji wa Soko la Kubadilishana Bidhaa (Commodities Exchange Market) ili kuepuka muingiliano unaoweza kutokea wa jitihada zinazofanana.
  4. Ushirikishe Ofisi ya Rais Usimamiaji na Ufuatiliaji wa Utekelezaji Program na Miradi ya Maendeleo (Presidential Bureau Delivery).

Baada ya mkutano huo, Katibu Mkuu Kiongozi alitembelea na kuona maeneo ya miradi miwili. Mradi wa ujenzi wa mnara wilayani Siha na mradi wa ujenzi wa Soko la Kimataifa la Nafaka Lokolova.

Balozi Sefue alihitimisha ziara yake hiyo kwa kukutana na Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Moshi na Wilaya zake. Katika kikao hicho, alirejea msisitizo wake kuwa, Watumishi wa Umma wawahudumie wananchi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na unyenyekevu mkubwa ili waweze kutoa taswira nzuri ya Serikali kwa wananchi. "Kwa nafasi yenu ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais na Serikali yake katika ngazi za kila mmoja wenu. Hivyo, mnawajibu wa kujua mnaowahudumia wanasemaje kuhusiana na huduma mnayotoa". Alisema.

Aidha, Balozi Sefue alitoa fursa kwa Watumishi kuuliza maswali, kutoa hoja na maoni kuhusiana na masuala ya kiutumishi wa umma yanayowatatiza katika utendaji wao wa kila siku. Maswali, maoni na hoja mbalimbali zilizotolewa na Watumishi zilijibiwa kwa ufasaha na Katibu Mkuu Kiongozi kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Bw. Jumanne A. Sagini pamoja na Watendaji alioambatana nao.

Katibu Mkuu Kiongozi anatarajia kuendelea na ziara za kukutana na Watumishi wa Umma katika mikoa yote.