Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, Ahimiza Wasomi Kuwa Mfano Wa Maadili Mema


KATIBU MKUU KIONGOZI, AHIMIZA WASOMI KUWA MFANO WA MAADILI MEMA

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 10/12/2015, amefungua Mdahalo kuhusu Maadili na Kuhimiza wasomi kuonyesha mfano mzuri katika kufundisha, kulinda na kuishi katika maadili mema kama viongozi, wazazi na sehemu ya jamii.

Akifungua Mdahalo huo ulioandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuadhimisha Siku ya Maadili Duniani, katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Sefue alihimiza Vyuo Vikuu na Taasisi zingine za Elimu kutambua wajibu na mchango mkubwa wa taasisi za elimu katika kuandaa wasomi na hatimaye watumishi na viongozi waadilifu, badala ya kuandaa mafisadi walioelimika. Alitoa wito kwa Taasisi hizo kupanda mbegu za maadili mema na kuzistawisha ndani ya mioyo ya wasomi wanaowasomesha badala ya vyuo hivyo kujivunia zaidi idadi ya wasomi wanaohitimu kwa kubobea katika taaluma mbalimbali. Alitoa pia rai kwa Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi zingine za Elimu kuamua ni jinsi gani vinaweza kuwachukulia hatua wahitimu wao wanaoaibisha vyuo hivyo kwa kutenda kazi zao kinyume kabisa na maadili ya utumishi wa umma na taratibu za taaluma zao.

Katika Mdahalo huo uliohudhuriwa na Wasomi, Watumishi wa Umma, Viongozi wa Siasa na Viongozi wa Dini, Balozi Sefue aliwahakikishia washiriki wa mdahalo huo kuwa serikali Kwa upande wake inaimarisha na itaendelea kuimarisha utendaji Serikalini na kupambana na maovu katika jamii, hususan rushwa na utovu wa maadili. Katika kutimiza azma hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alieleza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua thabiti za kuzuia viongozi na watumishi wa umma kutumia nafasi zao kujitajirisha, kujilimbikizia mali na kujipatia manufaa binafsi isivyo halali. “Tuko tayari kutunga Sheria mpya, kurekebisha zile zilizopo na kujenga mifumo mizuri ya usimamizi wa uadilifu, uwajibikaji, uwazi na mapambano dhidi ya rushwa”, alisema Balozi Sefue.

Aidha, alitoa wito kwa sekta binafsi kufanya biashara zao kwa kufuata maadili mema na kuendelea kusaini Hati ya Uadilifu kwa sekta binafsi, ahadi ambayo licha ya kuchochea ari na utashi wa aliyesaini hati hiyo kuishi na kuenenda katika misingi ya uadilifu, inaimarisha sana mapambano ya kisheria dhidi ya rushwa na makosa mengine kama hayo. Katika suala hili, Balozi Sefue alieleza wana mdahalo kuwa siku za usoni, Serikali haitakubali kufanya biashara, kwa kutoa zabuni au vinginevyo, na kampuni ambayo viongozi wake wanapata kigugumizi kusaini Hati ya Ahadi ya Uadilifu.

Katibu Mkuu Kiongozi alimalizia hotuba yake kwa kuwaomba wananchi kutoa taarifa serikalini wanapoona dhahiri kuwa utajiri alionao mtumishi wa Umma au Kiongozi wa Kisiasa haulingani na kipato chake halali.

NB: Soma hotuba kamili kwenye tovuti hii