Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE AHIMIZA MATUMIZI YA TAKWIMU NA TAARIFA SAHIHI KATIKA UANDAAJI WA NYARAKA ZA BARAZA LA MAWAZIRI, 15 JUNI, 2015
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue leo 15 Juni, 2015 amewahimiza Watendaji Waandamizi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na Waratibu wa shughuli za Baraza la Mawaziri kutumia takwimu na taarifa sahihi katika kuandaa nyaraka za Baraza la Mawaziri.
Balozi Sefue alikuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri iliyowakutanisha pia Waratibu wa Shughuli za Baraza la Mawaziri kutoka wizara mbalimbali.
Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika ukumbi wa St. Gaspar, Dodoma umelenga kuwanoa uwezo wa watendaji hao kuratibu shughuli za Baraza la Mawaziri pamoja na kuimarisha mahusiano miongoni mwao. Aidha, mkutano huo unatoa fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu, ujuzi na maarifa na pia ni fursa nzuri ya kufanya tathimini ya kazi na utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita.
“Shughuli za Baraza la Mawaziri ni za kikatiba, zinamuhusu Rais moja kwa moja, na zinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza cha kila waziri na kila wizara. Ni wajibu wenu pamoja na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, kutambua kuwa kazi mnazofanya ni sehemu ya mchakato wa kumsaidia Rais kufanya maamuzi sahihi. Hivyo, toeni umuhimu mkubwa na uzito unaostahili kwenye kutekeleza wajibu wenu. Tumieni weledi na maarifa yenu yote na muwe makini sana. Boresheni uwezo wa kiuandishi, iwe kwa Kiingereza au Kiswahili. Hakikisheni kuwa taarifa zote na takwimu zote mnazozitumia katika kushauri, ni taarifa sahihi na zinazotoka katika vyanzo rasmi vinavyoaminika. Siku zote kumbukeni usemi huu “trust but verify”. Kumbukeni kuwa ukimpotosha Waziri wako, naye atampotosha Rais.”
N.B. Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti hii.