Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE AFUNGUA WARSHA MAALUM YA KUANDAA MKAKATI WA KITAIFA WA KUJENGA NA KUIMARISHA STADI ZA KAZI KATIKA SEKTA ZINAZOCHOCHEA UKUAJI WA UCHUMI NCHINI, DAR ES SALAAM 17 AGOSTI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 17 Agosti, 2015 amefungua Warsha maalum ya Wadau ya Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kujenga na Kuimarisha Stadi za Kazi katika Sekta Zinazochochea Ukuaji wa Uchumi Nchini. Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Wizara ya Kazi na Ajira na inafanyika katika Hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam.

 

Balozi Sefue ameeleza kuwa, Mkakati huo ni muhimu na umekuja wakati ambao unahitajika sana. Kutokana na umuhimu wake, amewataka wadau wanaoshiriki warsha hiyo, kuipa umuhimu unaostahili kazi hiyo. Akasisitiza kuwa Mkakati utakaoandaliwa sharti uzingatie mahitaji halisi ya sasa hapa nchini na duniani yanayotokana na mabadiliko ya haraka ya Kisayansi na Maendeleo ya Kiteknolojia.

Ni muhimu na lazima tuwe na programu za Stadi za kazi ambazo ni mtambuka na ambazo zitawawezesha wasomi wetu kuingia kwa urahisi katika Soko la ajira na pia kuweza kujiajiri, amesema.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi amebainisha changamoto mbalimbali ambazo zikishughulikiwa kikamilifu zinaweza kuzalisha ajira nyingi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Ameelezea baadhi ya changamoto hizo kuwa ni; ongezeko kubwa la idadi ya watu, hususan vijana, ongezeko ambalo haliendani na ukuaji wa uchumi, Ongezeko kubwa la idadi ya wanaokimbilia mijini, ongezeko kubwa la vijana wasio na stadi za kazi, mazingira yasiyo rafiki kwa uwekezaji kama vile urasimu usio wa lazima na kukosekana kwa ushirikiano wa dhati kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, wasomi wa Tanzania kukosa utamaduni wa kujituma katika kazi na tabia ya kulaumu tu, upungufu wa kimaadili na mfumo wa elimu usiokidhi mahitaji ya sasa ya kiushindani.

NB: Hotuba kamili inapatikana katika tovuti hii.