Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA TAKWIMU NA KUSISITIZA UMUHIMU WA MATUMIZI HURIA YA TAKWIMU KWA MAENDELEO YA NCHI. HARBOUR VIEW HOTEL DAR ES SALAAM, 8 OKTOBA, 2015
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 8 Oktoba, 2015 amefungua Mkutano wa Wadau wa Takwimu na kusisitiza umuhimu wa matumizi huria ya takwimu kwa maendeleo ya nchi.
Katibu Mkuu Kiongozi, alialikwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kufungua mkutano huo uliojumuisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadiliana na kukubaliana namna bora ya kutumia takwimu kupima utekelezaji wa Mpango mpya wa Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals (SDGs) kwa miaka 15 ijayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi Sefue alieleza wadau wa mkutano kuwa, kwa kutambua umuhimu wa takwimu kwa maendeleo endelevu, Sheria mpya ya Takwimu, imeongeza nguvu, uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya takwimu katika nyanja zote za maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa jamii na utawala bora.
Balozi Sefue pia amehimiza wadau wa takwimu kujipanga ipasavyo na kukubaliana jinsi ya kuweka viashiria vya kupima Mpango huo mpya wa Maendeleo Endelevu ya duniani kwa uwazi, na haraka zaidi.
Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali, wakuu wa taasisi za umma na binafsi, wanataaluma na wawakilishi wa taasisi za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.
NB: Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika Tovuti hii.