Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE AFUNGUA KONGAMANO LA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NA KUSISITIZA KUWA UTATUZI WA CHANGAMOTO NYINGI ZA KIMAENDELEO UTATEGEMEA JINSI UTUMISHI WA UMMA ULIVYOJIPANGA NA KUWEZESHWA KUTEKELEZA WAJIBU WAKE, DAR ES SALAAM. 17 JUNI, 2015.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 17 Juni, 2015 amefungua Kongamano la siku moja la kuadhimisha Wiki ya Utumishi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwakaa huu yamebeba kaulimbiu isemayo: Utumishi wa Umma Katika Bara la Afrika ni Chachu ya Kuwawezesha Wanawake, Kuongeza Ubunifu na Kuboresha Utoaji Huduma kwa Umma”.

Chimbuko la kaulimbiu hii ni Azimio la Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 31 Januari, 2011, azimio ambalo lilitambua mchango wa mwanamke katika kuongeza ubunifu na hatimaye kuboresha utoaji huduma kwenye Utumishi wa Umma.

Balozi Sefue amesema, “Matarajio yangu ni kuwa mtapata fursa ya kujadili kwa kina na kuibua michango na mawazo mapya ya washiriki wa Kongamano hili, na kubaini fursa zilizopo katika kujenga uwezo wa wanawake na kutumia uwezo na ubunifu wao katika kutoa huduma bora kwa wananchi”.

“Wanawake wananafasi kubwa katika Uongozi na katika Utumishi wa Umma”, aliongeza. Na akaeleza kuwa dhamira ya kuleta usawa wa kijinsia kwenye uongozi, kwa maana ya nafazi za maamuzi ya kisiasa, na uongozi kwa maana ya Utumishi wa Umma, ni dhamira ya kweli kama ilivyojidhihirisha kwenye Katiba inayopendekezwa.

Aidha, Balozi Sefue amehimiza kuwa watumishi wanawake wanapopewa nafasi wahakikishe wanadhihirisha kwa vitendo na tabia kuwa wamestahiki madaraka waliyopewa na wanastahiki madaraka makubwa zaidi na kwa maneno wasione haya kuonesha uwezo wao.

 

N.B. Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana kwenye tovuti hii.