Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, AFUNGA MKUTANO WA FARAGHA WA MWAKA (ANNUAL RETREAT) WA MAKATIBU WAKUU NA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA. ST. GASPAR, DODOMA, 23 JULAI, 2015.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 23 Julai, 2015 amefunga rasmi Mkutano wa Faragha wa Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Mtakatifu Gaspar, mjini Dodoma.

Mkutano huo wa siku mbili umejadili masuala mbalimbali yanayohusu Utumishi wa Umma hususan wajibu wa Watendaji Wakuu Serikalini na Watumishi wengine kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Tumekubaliana kuhusu wajibu na haki za Watendaji Wakuu pamoja na Watumishi wa Umma kwa ujumla tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, alisema.

Balozi Sefue alieleza kuwa Mkutano umeazimia kuwa Watendaji Wakuu wanao wajibu mkubwa wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Uchaguzi Mkuu. Hivyo, wanapaswa kuzisimamia na kuzitumia pale ambapo zitakiukwa na baadhi ya Watumishi walioamua kwenda kushindania nafasi za kisiasa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama ili hatimaye tuwe na Uchaguzi mzuri na wa amani na utulivu.

Vilevile, alipongeza jitihada za Tume ya Uchaguzi kwa kazi nzuri ya uandikishaji wa wapiga kura na akahimiza Tume hiyo ifanye vizuri zaidi kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na mapungufu.

Mwisho, Katibu Mkuu Kiongozi alirejea kuwapongeza Watumishi wote wa Umma wanaoendelea kutekeleza majukumu yao vizuri na akawataka wachache wanaofanya vibaya kujirekebisha au la hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.