Habari
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue afanya ziara ya kikazi Mkoani Singida, tarehe 27 Juni, 2014.
KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE AFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI SINGIDA, TAREHE 27 JUNI, 2014.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue amefanya ziara ya kikazi Mkoani Singida tarehe 27 Juni, 2014 akiambatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Wakurugenzi kutoka TAMISEMI na Watendaji wa Ofisi ya Rais Ikulu.
Ziara hiyo ambayo ni mojawapo ya ziara anazofanya Katibu Mkuu Kiongozi kwenye Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa, ililenga pamoja na mambo mengine kumwezesha kujionea, kusikia na kubadilishana taarifa muhimu na Watendaji wa Sekretarieti ya Mkoa, Watumishi wa Sekretarieti na Halmashauri ya Mji wa Singida pamoja na Taasisi nyingine za Umma Mkoani humo.
Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kuzungumza na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa, Watumishi wa Sekretarieti na Halmashauri ya Mji wa Singida.
Katika Mkutano wake na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa, Watumishi wa Sekretarieti na Halmashauri ya Mji wa Singida, Katibu Mkuu Kiongozi alifafanua masuala mbalimbali ya Kisera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, ambapo pia alitoa maelekezo kwa Menejimenti na Watumishi wa Sekretarieti kuhusu namna Utumishi wao unavyopaswa kuwa. Vilevile aliwakumbusha umuhimu wa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Kiongozi alihimiza matumizi ya TEHAMA, ambapo alibainisha wazi kuwa hayakwepeki katika karne hii ya 21. Pia, alisisitiza kuhusu utunzaji wa siri za Serikali, matumizi ya mifumo ya kimenejimenti iliyowekwa, kuzingatia upandishaji vyeo watumishi wanaostahili, matumizi ya mfumo wa wazi wa upimaji wa utendaji kazi (OPRAS) na nidhamu kazini.
Mwishoni mwa ziara yake hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Mkoa wa Singida, ambapo alifurahishwa sana na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana hospitalini hapo. Hospitali hiyo imekuwa ikijipatia tuzo mara nyingi kutokana na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kutembelea mradi wa ujenzi wa Hopitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo umefikia hatua nzuri na ya kuridhisha. Kwa mujibu wa uongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Singida, hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa mikoa sita (6) iliyo karibu na mkoa huo.