Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI Y. SEFUE, AFANYA MKUTANO NA WAFANYAKAZI WA TAZARA NA KUWAELEZA JUU YA UAMUZI ULIOFANYWA NA SERIKALI KULIPA MISHAHARA YAO NA KUGHARAMIA MPANGO WA MAENDELEO YA TAZARA, DAR ES SALAAM, TAREHE 17 OKTOBA, 2015
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 17 Oktoba, 2015 amefanya mkutano na wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo, jijini Da es Salaam.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu Kiongozi alisikiliza risala na madai mbalimbali ya wafanyakazi hao yaliyowasilishwa kupitia uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) na madai mengine yaliyowasilishwa na wafanyakazi, na aliahidi kuyatafutia ufumbuzi.
Akieleza juu ya adha kubwa wanayopata wafanyakazi hao kwa kutolipwa mishahara yao kwa wakati na mwajiri wao TAZARA, Balozi Sefue alieleza na kuthibitisha uamuzi uliochukuliwa na Serikali wa kulipa mishahara ya wafanyakazi hao. Alieleza kuwa tayari Serikali imeanza kulipa mishahara hiyo na itaendelea kufanya hivyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa matarajio kuwa baada ya hapo, TAZARA itakuwa ina uwezo wa kujiendesha yenyewe.
Katibu Mkuu Kiongozi pia aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali imetenga shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kugharamia mpango wa maendeleo wa TAZARA. Kupitia mpango huo, Serikali imefanya uamuzi wa kukarabati vichwa vya treni, kugharamia ununuzi wa mafuta ya kuendeshea treni, na kukarabati miundombinu muhimu ya reli hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dkt. Shaban Mwinjaka na viongozi wengine wa wizara hiyo. Menejimenti ya TAZARA iliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Ronald Phiri.
NB: Hotuba kamili ya Katibu Mkuu Kiongozi inapatikana katika tovuti hii