Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI, BALOZI OMBENI SEFUE AANZA ZIARA YA KIKAZI KATIKA MKOA WA PWANI NA MIKOA YA KANDA YA KASKAZINI, 15 SEPTEMBA, 2014.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, leo tarehe 15 Septemba, 2014 ameanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Pwani na mikoa ya Kanda ya kaskazini ambayo ni Tanga, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake hiyo, Balozi Sefue ametembelea mkoa wa Pwani na kukutana na Menejimenti ya Sekretarieti ya mkoa na wilaya zake pamoja na Watendaji wa Taasisi za Umma na Wakala za Serikali zilizopo mkoani humo, vile vile Katibu Mkuu Kiongozi aliongea na baadhi ya Watumishi wa kada mbalimbali waliopo katika Sekretarieti ya mkoa na waliopo katika Taasisi za umma na Wakala za Serikali mkoani Pwani.

Katika kikao chake hicho Katibu Mkuu Kiongozi aliwakumbusha watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma. Pia, alieleza kuw, Watumishi wa Umma wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na kwa kuzingatia matokeo (Results Oriented), alikadhalika aliwaasa Watumishi kusikiliza matatizo ya wananchi na kuwahudumia kwa wakati bila kuwazungusha.

Katika ziara yake hii Katibu Mkuu Kiongozi ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Abdallah Sagini, Maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Ikulu na baadhi ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI.

Katibu Mkuu Kiongozi anatarajia kumaliza ziara yake hiyo tarehe 19 Septemba, 2014.