Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John W.H. Kijazi, leo tarehe 9 Machi, 2016 amekutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi, Balozi Kari Alanko.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John W.H. Kijazi, leo tarehe 9 Machi, 2016 amekutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi, alipomtembelea Ofisini kwake akifuatana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Joseph Semboja na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Pekka Hukka.

Kwa ujumla, mazungumzo hayo yalihusu maendeleo ya Taasisi ya Uongozi iliyoanzishwa na Serikali za Tanzania na Finland mwaka 2010 kwa lengo la kuwajengea Viongozi wa Tanzania na Afrika, uwezo wa kumudu majukumu yao vema na kwa ufanisi zaidi.

Katibu Mkuu Kiongozi aliishukuru Serikali ya Finland kwa kuendelea kuwa mbia muhimu wa maendeleo wa Tanzania, sio tu kupitia Taasisi ya Uongozi bali pia kupitia miradi mbalimbali inayoifadhili nchini. Alisema uwekezaji wa Serikali zetu mbili umeiwezesha Taasisi ya Uongozi kupata mafanikio na heshima kubwa barani Afrika na duniani. Aliongeza kuwa, ndio maana nchi hizo zimedhamiria kuwekeza zaidi na kufungua milango kwa wabia wengine, ili kuimarisha Taasisi hiyo na kuiwezesha kuhudumia washiriki kutoka katika nchi nyingi za Afrika.

Kuhusu uwekezaji wa Serikali ya Tanzania katika Taasisi ya Uongozi, Katibu Mkuu Kiongozi alizungumzia uamuzi wa Serikali wa kutoa kiwanja kwa ajili ya kujenga maskani ya kudumu ya Taasisi hiyo katika mji wa Bagamoyo. Vilevile, alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania inachangia zaidi ya asilimia 40 za gharama za uendeshaji wa Taasisi hiyo. Aliongeza pia, katika jitihada za kuhakikisha kuwa Taasisi ni mradi endelevu, Serikali imepeleka zaidi ya Watumishi 1,600 kupata mafunzo katika Taasisi hiyo.

Kwa upande wa Serikali ya Finland, Balozi Alanko alisema kuwa pamoja na mikakati ya kubana matumizi, Serikali mpya ya nchi hiyo, iliyoingia madarakani mwezi Juni, 2015, imetoa kipaumbele kwa Tanzania kuendelea kupata misaada ya maendeleo na fursa kwa makampuni ya Finland kuwekeza nchini. Aidha, ameahidi kuwa Bodi ya Taasisi ya Uongozi itaendelea kushirikiana na Menejimenti ya Taasisi kuhakikisha kuwa inatekeleza matakwa ya nchi washirika (Tanzania na Finland).

Kwa sasa Bodi hiyo na wadau wake, ipo katika mchakato wa kuandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano 2016/17 – 2021/22 ambao utalenga kupanua wigo wa huduma za Taasisi hiyo, ili kuzifikia nchi nyingi zaidi za Afrika na kuweka msisitizo katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan katika eneo la Utawala Bora.