Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein A. Kattanga asaini kitabu cha maombolezo katika ofisi ya ubalozi wa Japan.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein A. Kattanga leo tarehe 16 Julai, 2022 majira ya saa 8 machana amefika katika ofisi za ubalozi wa Japan jijini Dar es Salaam kusaini kitabu cha maombolezo Ubalozi kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu wa nchi hiyo Shinzo Abe aliyeuawa kwa kupigwa risasi nchini humo tarehe 8 Julai, 2022. 

Mara baada ya kufika katika ofisi za Ubalozi huo zilizopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi alipokelewa na mwenyeji wake Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Misawa Yasushi na moja kwa moja walielekea ofisini kwake kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo.

Mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, Balozi Kattanga alimweleza Balozi Yasushi kuwa alishtushwa sana mara baada ya kupata taarifa za kifo cha waziri mkuu mstaafu Shinzo Abe kufuatiwa kupigwa risasi na mmoja wa watu waliokuwa wakimsikiliza kiongozi huyo alipokuwa akihutubia katika mkutano wa kampeni katika mji wa Nara uliopo kusini mwa kisiwa cha Honshu ambacho ndio kikubwa kati ya visiwa vinne (4) vikubwa vinavyounda nchini hiyo.

“Mimi binafsi, serikali ya Tanzania pamoja na watanzania kwa ujumla tumesikitishwa sana na kifo cha kiongozi wenu ambacho kimetokea pasipo kutegemea kwa mazingira ya Japan, pole kwa watu wa Japan na familia yake”, alisema Balozi Kattanga.

Kwa upande wake Mhe. Misawa alimshukuru Balozi Kattanga kwa ujio wake huo, pamoja na ushirikiano wa kiutendaji kwa serikali za nchi zote mbili yaani Tanzania na Japan ambao ofisi yake imekuwa ikitekeleza na kuusimamia.

Mwisho Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na ujumbe wake waliagana na Balozi Misawa pamoja na maofisa wengine wa ubalozini hapo na kurudi ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam kuendelea na majukumu yake.