Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi azungumza na Wafanyabiashara Wakubwa wa Afrika Mashariki


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, jana tarehe 1 Machi, 2016 alimuwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika chakula cha usiku, kilichoandaliwa na Baraza la Wafanyabiasha la Afrika Mashariki (EABC) katika Hotel ya Mount Meru, Arusha.

Hafla hiyo, ilihitimisha Mkutano wa Wafanyabiashara Wakubwa wa Jumuiya hiyo (Business Leaders Summit) uliofanyika siku moja kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na mengine, ulitoa fursa kwa wanachama wa EABC na wadau wa sekta ya biashara kujadili changamoto na kuandaa mapendekezo ya namna zinavyoweza kutatuliwa na watunga sera (policy makers) na wafanya maamuzi (decision makers) wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alielezea shahuku aliyokuwa nayo Mheshimiwa Rais ya kukutana na wafanyabiashara hao, japo hakuweza kufanya hivyo kutokana na majukumu mengine muhimu yanayomkabili kama Mwenyekiti wa EAC.

Katibu Mkuu Kiongozi alibainisha pia kuwa, Rais Magufuli ni rafiki wa Wafanyabiashara na anatambua umuhimu wao katika ujenzi wa uchumi imara na harakati za kupunguza umaskini wa kila hali. Miongoni mwa masuala aliyomuagiza kuyafafanua kwa wafanyabiashara hao ni:

· Dhamira ya Tanzania ya kuendeleza mchakato wa utangamano na kuenzi mchango wa sekta binafsi ambayo ni mdau muhimu katika mchakato huo;

· Vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano vinavyoendana na malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na vyenye kutoa fursa kwa wafanyabiashara walio kwenye Jumuiya;

· Wajibu mbalimbali wa sekta binafsi katika ujenzi wa Jumuiya yenye maendeleo endelevu, amani na utulivu na ambayo watu wake wote wanaheshimu maadili na kuchukizwa na rushwa na ufisadi.

N.B: Hotuba kamili inapatikana kwenye tovuti hii.