Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi azindua Mfumo wa kuzuia simu zilizoibiwa na zisizokidhi viwango vya ubora kutumika nchini Tanzania. 17 Disemba, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 17-12-2015 amezindua mfumo maalum wa Rajisi ya Namba za Utambulisho za Simu za Kiganjani ambao utazuia simu zilizoibiwa na zile zisizokidhi viwango vya ubora unaokubalika kimataifa kutumika hapa nchini.

Uzinduzi wa mfumo huo ujulikanao kama 'CEIR' unalenga kupunguza au kumaliza kabisa tatizo lililoshamiri la wizi wa simu za viganjani, uuzaji na ununuzi wa simu zisizokidhi viwango vya ubora na matumizi ya simu kinyume na malengo mema.

Wakati wa uzinduzi huo, Balozi Sefue alitoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha kuwa laini ya simu yake imesajiliwa kwa taarifa za ukweli zinazomhusu. Aidha alitoa rai watanzania kuachana na tabia ya kununua simu zisizokidhi viwango vya ubora kwa madai ya urahisi wa bei kwa kuwa zipo pia simu za bei rahisi lakini zina ubora unaokubalika kimataifa.

Hafla ya uzinduzi wa mfumo huo ilifanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na kuhudhuriwa na watendaji wakuu wa serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dkt. Ally Y. Simba, akitoa maelezo juu ya ufanisi na faida za mfumo huo, alibainisha kuwa pamoja na kuweka usalama wa matumizi ya simu za kiganjani, mfumo huu pia utawezesha serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweza kufahamu kiasi cha mapato kinachoingizwa na makampuni ya mawasiliano kupitia mauzo yao ya muda wa maongezi pamoja na tozo linalotokana na kutuma au kupokea fedha na kufanya malipo kupitia mitandao mbalimbali.

Naye Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Bw. Innocent Mungy, alisema Serikali kupitia mamlaka hiyo kuanzia leo 17 Disemba, 2015, itaanza kutoa elimu kuelimisha jinsi ya kutambua na kuhakiki ubora wa simu na utaratibu utakaotumika kutoa taarifa zitakazowezesha simu iliyoibiwa kufungwa ili isitumike tena. Bw. Mungy alijulisha kuwa Mamlaka imetoa kipindi cha miezi sita (6) kuruhusu wananchi kuelewa mfumo huo na kuepukana na usumbufu unaoweza kutokea kabla ya kufunga rasmi simu hizo mwezi Juni mwakani.

NB: Soma Hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi katika tovuti hii.