Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI AWASILISHA MADA KUHUSU MASUALA YA UONGOZI WA KITAIFA KATIKA CHUO CHA TAIFA CHA ULINZI (NDC), KUNDUCHI, 28 APRILI 2015
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 28 Aprili, 2015 amewasilisha mada inayohusu masuala ya uongozi wa kitaifa mbele ya washiriki ambao ni Viongozi Waandamizi Wakuu wa Serikali wanaohudhuria Kozi ya Muda Mfupi (Capstone Course) katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College - NDC) kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam. Kozi hiyo mahsusi ilifunguliwa tarehe 27 Aprili, 2015 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dk. Hussein A. Mwinyi (MB) na itahitimishwa tarehe 30 Aprili, 2015.
Balozi Sefue alielezea misingi ya uongozi wa kitaifa na mfumo wa ufikiaji wa maamuzi yanayolihusu taifa. Aidha, alidadavua kuhusu mfumo wa utayarishaji wa Sera za Taifa unaotumika nchini, huku akibainisha pia changamoto zilizopo na namna ya kuzishughulikia.
Katibu Mkuu Kiongozi ameendelea kusisitiza zaidi suala la kubadilika kifikra (mindset) katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya kitaifa na kuhimiza kuwepo kwa vitendo kwa dhana ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utekelezaji na pia kuzingatia misingi ya utendaji kazi inayojali ufanisi na matokeo.
NB: Wasilisho la Katibu Mkuu Kiongozi linapatikana katika tovuti hii.