Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AWAKARIBISHA WATUMISHI WAPYA IKULU, AWAAGA WATUMISHI WASTAAFU NA KUWAPONGEZA WAFANYAKAZI BORA NA WANAMICHEZO WA IKULU SPORTS CLUB, 21-11-2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 21 Novemba, 2014, amewakaribisha watumishi wapya wa Ikulu, amewaaga watumishi wastaafu wa Ikulu na kuwapongeza wafanyakazi bora na wanamichezo wa Ikulu Sports Club kwa ushindi mkubwa walioupata wakati wa Mashindano ya 34 ya SHIMIWI yaliyofanyika mwezi Septemba mwaka huu, mjini Morogoro. Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.

Akiwakaribisha watumishi wapya wa Ikulu, Katibu Mkuu Kiongozi aliwapongeza kwa uteuzi wao na kuwakaribisha Ikulu, akisisitiza kuwa uteuzi wao umetokana na utendaji kazi wao unaoridhisha na kuaminiwa, hivyo wanapaswa kuuendeleza katika kituo chao kipya cha kazi. “Kazi ya kumhudumia Rais inahitaji Uaminifu, Uadilifu na Weledi mkubwa”, alisisitiza.

Akiwapongeza watumishi wastaafu wa Ikulu, Balozi Sefue aliwasifu kwa utumishi wao uliotukuka na kwa kuhitimisha utumishi wao wa umma huku wakiacha kumbukumbu nzuri ya kiutendaji na ya kuigwa na watumishi waliobaki. Aidha, aliwatakia wastaafu hao afya njema, maisha mazuri na mafanikio katika hatua hii nyingine ya maisha na akaahidi kuwa ofisi na watumishi wataendelea kuwakumbuka kwa yale yote mazuri waliyoyaacha na akawasihi kuwa kila itakapowezekana wasiache kutoa ushauri na uzoefu kadri watavyoombwa.

Kwa upande wa wafanyakazi bora, Katibu Mkuu Kiongozi aliwapongeza sana wafanyakazi hao kwa kuchomoza na kuwa bora miongoni mwa wenzao wengi. Alieleza kuwa kuchaguliwa kwao kunaonyesha jinsi wafanyakazi wenzao wanavyothamini kiwango cha mchango wao katika Ofisi ya Rais, Ikulu. Hata hivyo aliwaasa kuwa wasibweteke na mafanikio waliyoyapata na badala yake yawe ni chachu ya kufanya vizuri zaidi, akirejea msemo usemao “Mgema akisifiwa, tembo hulitia maji”.

Halikadhalika aliwahimiza watumishi wengine kuendelea kujituma kwa bidii na maarifa katika utendaji wao wa kazi ili na wao waweze kushika nafasi ya ufanyakazi bora kwa siku zijazo.

Akiwapongeza wanamichezo wa Ikulu Sports Club, Katibu Mkuu Kiongozi alielezea furaha yake kutokana na ushindi wa jumla ya vikombe sita (6) ambavyo walivinyakua. Balozi Sefue alisisitiza kuwa kushiriki michezo na kufanya mazoezi ya viungo kwa ujumla ni muhimu sana kwa afya ya kila mmoja wetu na akarejea rai aliyoitoa mwaka jana kuwa hata kama muda ni finyu, watumishi watafute muda wa kufanya mazoezi mepesi kama vile kutembea mara kwa mara, na hiyo iwe ratiba yao ya kila siku.

Mwisho, Katibu Kiongozi aliupongeza Uongozi wa TUGHE katika Ofisi ya Rais, Ikulu, kwa ushirikiano wao mzuri na Ofisi ya Rais, Ikulu, ambao unawezesha mashauriano kwa kila jambo, badala ya misuguano sehemu za kazi na akahimiza ushirikiano huo uimarishwe zaidi.

Hafla hiyo iliambatana na utoaji zawadi mbalimbali kwa makundi hayo. Aidha, watumishi wastaafu, pamoja na zawadi, walipokea Vyeti vya utumishi uliotukuka.