Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AWAAGA MAKATIBU WAKUU NA NAIBU MAKATIBU WAKUU WASTAAFU, 9 OKTOBA, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 9 Oktoba, 2015, amewaandalia hafla ya kuwaaga Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu waliostaafu nafasi zao kwa nyakati mbalimbali.

Jumla ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kumi na saba (17) waliagwa katika hafla hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.

Balozi Sefue amewapongeza wastaafu hao kwa utumishi wao uliotukuka na ambao uliwawezesha kustaafu kwa staha na heshima kubwa.

Aidha, alieleza kuwa pamoja na kuwa wastaafu hao wametengana na Watumishi wengine wanaoendelea katika utumishi wa umma, kustaafu kwao bado kumekuwa ni jambo la heri kwani wametoa mwanya kwa watumishi wengine kupandishwa vyeo kuchukua nafasi zao na hivyo kufanikisha dhana nzima ya kurithishana madaraka.

Vilevile, amewaasa wastaafu hao kuendelea kujishughulisha na shughuli mbalimbali na kwamba kwa kufanya hivyo kutawajenga kiafya na kifikra.

Akaeleza kuwa ni kwa mantiki hiyo, Serikali imekuwa ikiwatumia wastaafu hao katika nafasi mbalimbali zinazohitaji weledi, uzoefu na ujuzi wao.

 

NB: Soma hotuba kamili katika tovuti hii.