Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi atunuku Shahada kwa wahitimu, Chuo cha Takwimu


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 19-12-2015 amekuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki na kutunuku Shahada ya Kwanza ya Takwimu Rasmi (Bachelor of Official Statistics) kwa wahitimu 29 wa Chuo hicho.

Akizungumza katika mahafali hayo, Balozi Sefue amevitaka Vyuo na Taasisi za Elimu nchini kuhakikisha vinaelewa ipasavyo mahitaji ya jamii na soko la ajira na kisha kutoa elimu inayoendana na mahitaji hayo.

Balozi Sefue pia aliwataka wahitimu wa elimu ya juu kuwa mfano mwema wa kutenda kazi kwa bidii, uadilifu, uzalendo na uaminifu. Aliwahimiza wahitimu kuacha tabia iliyozoeleka kwa wengi ya kutokuendelea kusoma vitabu baada ya kuhitimu masomo yao na badala yake aliwataka kuendelea kuongeza maarifa yao kwa kujisomea vitabu na majalada mbalimbali.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Profesa Moris Mbago na Mkuu wa Chuo cha Takwimu Profesa Innocent Ngalinga walimueleza Katibu Mkuu Kiongozi changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho na kuainisha mikakati ya kukabiliana nayo.

Katibu Mkuu Kiongozi aliueleza uongozi wa Chuo hicho pamoja na wahitimu wa mahafali hayo ya kwanza kwa ngazi ya Shahada katika taaluma ya Takwimu Rasmi, kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana kushirikiana na Chuo hicho kukabiliana na changamoto zinazokikabili. Aliipongeza Chuo hicho kwa kutimiza miaka 50 tangu kianzishwe na mchango mkubwa inayotoa kuelimisha watakwimu wa ngazi mbalimbali hapa nchini na katika Bara la Afrika.

NB: Soma hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi katika tovuti hii