Habari
Katibu Mkuu Kiongozi atembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi mpya za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. 7 Septemba, 2016
Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Mhandisi John W. H. Kijazi, leo tarehe 7 Septemba, 2016
ametembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na baadaye alipata fursa ya kutembelea
mradi wa ujenzi wa Ofisi mpya za Mkuu wa Mkoa iliyopo eneo la Kilimani mjini
Dodoma.
Akiwa katika
Ofisi za Mkuu wa Mkoa, Katibu Mkuu Kiongozi alipokea taarifa ya Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa
Jordan Rugimbana kuhusu maandalizi
ya Serikali kuhamia Dodoma, ambapo Mkuu wa Mkoa alitaarifu kuwa maandalizi
yanaendelea vizuri na kwamba Uongozi wa Mkoa na Wananchi wa Dodoma wamejipanga
vilivyo kupokea wageni mbalimbali kutoka Dar es Salaam na maeneo mengine ya
Tanzania watakaohamia Dodoma.
Kikao hicho
kifupi kiliudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Wajumbe wengine wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma. Akiongea katika Kikao hicho,
Katibu Mkuu Kiongozi aliwapongeza kwa maandalizi hayo na kuahidi kuendelea
kuwapatia ushirikiano. Aidha, alisisitiza umuhimu wa uratibu mahiri wa wadau
wote wanaoshiriki katika mchakato wa maandalizi ya Serikali kuhamia Dodoma ili
kupata matokeo makubwa zaidi katika maeneo yote ya mpango huo.
Baada ya
kumalizika kwa Kikao hicho, Katibu Mkuu Kiongozi alitembelea mradi wa ujenzi wa
Ofisi mpya za Mkuu wa Mkoa inayojengwa katika eneo la Kilimani mjini Dodoma. Akiwa
katika mradi huo Katibu Mkuu Kiongozi alieleza kufurahishwa kwake na ubunifu wa
jengo hilo pamoja na hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo. Aidha, alimwahidi
Mkuu wa Mkoa kuwa Ofisi yake itatoa ushirikiano utakaohitajika ili kuhakikisha
ujenzi huo unakamilika mapema.
Kufuatia
ziara hiyo Katibu Mkuu Kiongozi, alifanya ziara nyingine kwenye Kituo cha Taifa
cha Kumbukumbu na Nyaraka kilichopo eneo la Kisasa mjini Dodoma ambapo alipata
wasaa wa kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi na Wafanyakazi wa Kituo hicho.
Mazungumzo hayo pia yalimshirikisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejiment ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo
cha Kumbukumbu Tuli, Bwana Firimin M. Msiangi.
Katibu Mkuu
Kiongozi aliupongeza Uongozi na Wafanyakazi wa Kituo hicho kwa kazi nzuri
wanayoendelea kuifanya katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, alisisitiza
umuhimu wa kuweka kumbukumbu muhimu kwa ajili ya matumizi ya sasa na baadaye ya
Serikali. Vilevile, aliwakumbusha watumishi wote kituoni hapo umuhimu wa kudumisha
uadilifu na maadili, ikiwa ni pamoja na kutunza siri za nyaraka zinazochujwa na
kutunzwa kituano hapo . Kadhalika, alisisitiza umuhimu wa Wizara, Idara na
Taasisi za Serikali kukitumia Kituo hicho kama ilivyokusudiwa. Mwisho aliahidi
kuwa Serikali itajitahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazokikabili
Kituo hicho na watumishi wake.