Habari
Katibu Mkuu Kiongozi atembelea na kukagua eneo utakapojengwa Mji wa Kisasa wa Serikali, Ihumwa Mjini Dodoma. 23/11/2017

KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA NA KUKAGUA ENEO UTAKAPOJENGWA MJI WA KISASA WA SERIKALI, IHUMWA MJINI DODOMA. 23/11/2017
Na Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi na Makatibu Wakuu leo
wametembelea na Kukagua eneo utakapojengwa Mji wa Kisasa wa Serikali katika
eneo la Ihumwa Mjini Dodoma, ili kujionea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji
wa mradi huo.
Akizungumza katika eneo la mradi unaotarajiwa kutekelezwa katika eneo
lenye ukubwa ekari 1500 Balozi Kijazi amesema kuwa Mji huo utakuwa wa kipekee
na hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuhakikisha kuwa Makao Makuu ya nchi
yanakuwa katika mpangilio wa kisasa ili kuleta tofauti kati ya mji huo na miji
mingine.
“Niwatoe wananchi shaka kuhusu Serikali kuhamia Dodoma kwa kuwa dhamira
ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
imeshaanza kutekelezwa kwa vitendo na sehemu kubwa ya Watumishi wa Serikali wameshahamia
hapa Dodoma Wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu” . Alisisitiza
Balozi Kijazi
Akifafanua amesema kuwa mji huo utakuwa na maeneo kwa ajili ya
majengo ya Wizara, Taasisi, Balozi, na huduma mbalimbali za kijamii
ikiwemo Viwanja vya michezo, Hospitali, maeneo ya kupumzikia, Maeneo ya
Biashara .
Aliongeza kuwa upatikanaji wa huduma katika Mji wa Serikali utakuwa
wa uhakika na utakuwa umerahisishwa kutokana na kuwepo kwa Taasisi za
Serikali na Wizara zote katika eneo moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw.
Nehemia Mchechu amesema kuwa ni muhimu kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza mkoani
Dodoma kutokana na mipango ya Serikali kujenga mji huo wa Kisasa wa Serikali.
Aliongeza kuwa mawazo ya awali ya namna ya kujenga mji huo wa kisasa wa
Serikali yapo na kinachosubiriwa ni hatua mbalimbali za kiutendaji
zitakazowezesha kutekelezwa kwa mradi huo.
Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma umepata msukumo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na tayari utekelezaji wake unaendelea ambapo Mawaziri wote wameshahamia Dodoma, Makatibu Wakuu na Watumishi Wengine wa Serikali pia wameshahamia.