Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi atembelea mradi wa Reli ya kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro – 20/12/2021


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein A. Kattanga, leo tarehe 20/12/2021 amefanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR). Huu ni mojawapo ya miradi ya kimkakati ya kuimarisha uchumi wa chi ambao unajengwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Kiongozi aliambatana na wasaidizi katika ofisi yake pamoja na maofisa waandamzi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.

Ziara yake hiyo ilianzia katika eneo la stesheni ya reli zilizopo katikati ya jiji la Dar es Salaam. Mara baada ya kuwasili hapo Katibu Mkuu Kiongozi alilakiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wakiongozwa na Katibu Mkuu Uchukuzi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bw. Gabriel J. Migire, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mhandisi Masanja K. Kadogosa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo Prof. John Wajanga Kandoro, pamoja na baadhi ya Wataalam na Wafanyakazi wa Kampuni ya Yapi Merkezi ambao ndio wakandarasi wakuu wa mradi huo. Akiwa katika eneo hilo Balozi Kattanga alionyeshwa maeneo mbali mbali ya jengo la stesheni hiyo na kwa mujibu maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), jengo hilo tayari limekamilika na liko tayari kwa ajili ya matumizi kinachosubiriwa ni usimikaji wa vifaa na mifumo ya uendeshaji wa Reli hiyo ya kisasa. Katika jengo hilo Katibu Mkuu Kiongozi alijionea maeneo ya ukataji na uhakiki wa tiketi, maeneo ya kupumzikia abiria, maneo ya biashara, eneo la kupandia treni pamoja na chumba maalum cha kudhibiti mienendo ya treni katika njia zake (Control Room).

Baada ya kumaliza kukagua jengo hilo, msafara ulielekea stesheni ya Pugu iliyo takribani kilometa 27 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam. Mara baada ya kufika katika stesheni hiyo Katibu Mkuu Kiongozi alipata nafasi kuona jengo la stesheni eneo la ukataji na uhakiki wa tiketi, ni katika stesheni hii Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na ujumbe wake walianza safari ya kukagua Reli hiyo kwa kutumia usafiri wa Treni ya uhandisi inayotumiwa na Wahandisi na Wataalam wa Kampuni ya Yapi Merkezi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Wakiwa katika safari ya kukagua reli hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na ujumbe wake walipata fursa ya kupata maelezo ya hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa mradi huo pamoja na maendeleo ya shirika la reli Tanzania kwa ujumla. Maelezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Masanja Kadogosa akishirikiana na baadhi wa Maofisa waandamizi wa shirika hilo.

Katika maelezo yake Mhandisi Kadogosa aliweka bayana hatua zilizofikiwa katika sehemu kuu tatu za ujenzi wa Mradi huo ambazo ni:-

Njia ya Dar es Salaam mpaka Morogoro yenye urefu wa kilomita 205 za njia kuu na kilomita 95 njia za mapishano ambayo imekamilika kwa asilimia 94.78, njia hii ina jumla ya Stesheni 6 na karakana kubwa moja iliyopo eneo la Kwala.

Njia Morogoro mpaka Makutupora Dodoma yenye urefu wa kilometa 422 zikijumuisha kilometa 336 za njia kuu na 86 za njia za mapishano ambayo imekamilika kwa asilimia 77.03, njia hii ina jumla ya vituo 8 na karakana kuu moja (1) iliyopo katika stesheni ya Ihumwa.

Sehemu ya tatu ni njia kutoka Isaka mpaka Mwanza mjini yenye urefu wa kilomita 341 inayojumuisha kilomita 249 njia kuu na 92 za njia za mapishano ambayo mpaka sasa imekamilika kwa asilimia 4.

Kwa upande wa uboreshaji wa reli na miundombinu ya awali ya shirika, taarifa ya Mkurugenzi Mkuu  inaonyesha maeneo mbali mbali yanayoendelewa kuboreshwa ikiwa ni pamoja ununuzi wa mabehewa 44 ya abiria na injini 3 pamoja na kukarabati mabehewa 200 pia Shirika limeingia mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa ya mizigo 600 na ya abiria 37 ambao ukarabati huu unategemea kukamilika mwaka 2024.

Msafara huo pia ulipata nafasi ya kufika katika kituo kikubwa cha karakana na upangaji wa mabehewa ya mizigo (Marshalling Yard) cha Kwala kilichopo maeneo ya Vigwaza mkoani Pwani ambapo hapo Katibu Mkuu Kiongozi alipata nafasi ya kujionea shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo. Msafara huo wa Katibu Mkuu Kiongozi ulifikia tamati ya ziara yake katika stesheni ya Morogoro mjini ambapo mara baada ya kukagua jengo la stesheni hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa maagizo kwa uongozi wa Shirika kuangalia namna ya kujitanua kibiashara hasa kwa masoko ya Nchi za jirani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda na Burundi.

Mwishoni mwa ziara hiyo Katibu Mkuu Kiongozi alipata fursa ya kupiga picha za kumbukumbu na Watendaji wa Shirika la Reli pamoja na Wafanyakazi wa kampuni ya Yapi Merkezi