Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA MAONYESHO YA KILIMO KANDA YA KATI NZUNGUNI, DODOMA 07 AGOSTI, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue tarehe 7 Agosti, 2014 alitembelea maonyesho ya Kilimo ya mwaka 2014 Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzunguni Mjini Dodoma kujionea namna taasisi na makampuni mbalimbali yanavyotoa huduma katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi nchini.

Maonyesho hayo yanayofanyika kila mwaka yanatoa fursa mbalimbali kwa Taasisi za Umma, Wakala na Kampuni za Umma na zile za binafsi kwa wakulima na wafugaji kama vile Utaalamu na Ushauri kwa lengo la kuboresha Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.

Balozi Sefue aliwaeleza waandishi wa habari waliokuwa kwenye uwanja huo kuwa maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Wakulima wa hapa nchini kutoka katika kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha biashara na hivyo kujikwamua kimaisha kwa kutumia utaalamu, ushauri na miundo mbinu inayopatikana kwenye maonyesho hayo.

Aidha Balozi Sefue alisisitiza kuwa upo umuhimu wa kuendeleza mawasiliano baina ya Wadau wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi na taasisi zinazoshiriki kwenye maonyesho haya badala ya kuwasiliana tu wakati wa maonyesho.

Kaulimbiu ya Maonyesho ya Mwaka huu ni "MATOKEO MAKUBWA SASA - KILIMO NA MIFUGO NI BIASHARA".