Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI ATEMBELEA MAABARA YA WATAALAM WA SEKTA YA AFYA KATIKA MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA, 24-10-2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ametembelea maabara iliyowakutanisha Wataalam wa Sekta ya Afya kutoka Serikalini na Taasisi nyinginezo zinazojihusisha na masuala ya afya, iliyofanyika katika hoteli ya Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam.

Maabara za namna hii zimekuwa zikiendeshwa na Ofisi ya Rais Usimamizi wa Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), ambapo wataalam mbalimbali kutoka katika sekta zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango huo, hukutanishwa kwa takriban majuma sita (6), ili kupata nafasi ya kuchambua changamoto zilizopo katika sekta husika na kupendekeza namna ya kuzitatua katika mawasilisho ya mapendekezo hayo kwa Wadau wa sekta hizo kutoka Serikalini na Taasisi zisizo za Kiserikali kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wake.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Sefue alielezea kufurahishwa kwake na jinsi ambavyo wataalam hao walivyoainisha vipaumbele vilivyopo katika sekta ya afya ili vifanyiwe kazi ili kuboresha sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa jamii ya Watanzania.

Akitoa mchango wake Balozi Sefue alikubaliana na mapendekezo yaliyotolewa, ikiwa ni:-

         i.            Utumiaji wa Wataalam wa Sekta ya Afya waliostaafu lakini bado wana utaalam na nguvu ya kufanya kazi.

       ii.            Uandaaji mapema wa vijana wanaotarajia kujiunga na mafunzo na utumishi katika sekta ya afya.

      iii.            Uimarishaji wa usambazaji wa madawa na vifaa tiba katika vituo vya afya nchi nzima.

     iv.            Uimarishaji wa vituo vinavyotoa huduma ya afya.

       v.            Uimarishaji wa Huduma za mama wajawazito na watoto katika vituo vya afya.

     vi.            Mafunzo stahiki kwa Wataalam wa sekta ya afya

Kuhusu suala la mafunzo, Katibu Mkuu Kiongozi alishauri kuwa, pale inapowezekana mpango huo wa mafunzo utumie mfano wa nchi ya Cuba, ambapo wataalam wa afya hupewa mafunzo yanayolenga kutatua matatizo ya kiafya yaliyopo kwenye jamii wanazoishi na pia huandaliwa kuhudumia maeneo ambayo wanaishi ili kupunguza tatizo la baadhi ya wataalam kukwepa kwenda kuhudumia kwenye vituo vya kazi walivyopangiwa.

Pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, maabara hiyo ilitembelewa pia na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. George Yambesi, Mganga Mkuu wa Serikali, Dr. Donald Mbando na mwakilishi wa Katibu Mkuu TAMISEMI, ambao pia walikuwa na mchango wao katika uboreshaji wa mawasilisho yaliyofanywa na maabara hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa "BRN" Bw. Omari Issa, alipongeza na kuipokea michango iliyotolewa na watendaji hao wa Serikali na pia alitolea ufafanuzi mtindo wa kutumia maabara ambao umekuwa ukiwakutanisha wataalam kuchambua na kuibua maeneo ya kufanyiwa kazi katika sekta husika ambayo huingizwa katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, alisisitiza kuwa wataalam hao hufanya kazi kizalendo kwani hawalipwi posho yoyote wanapokuwa katika maabara hizo.

Mbali na Sekta ya Afya, mpango huu umeshajumuisha sekta za Kilimo, Maji, Elimu, Uchukuzi, Nishati, Uboreshaji wa mazingira ya biashara na Ukusanyaji wa mapato.

Mwishoni mwa kikao hicho Balozi Sefue aliwapongeza wataalam hao kwa kazi yao nzuri na kuahidi kuwa serikali ipo tayari kutoa msaada mkubwa katika kutekeleza maeneo ambayo yamependekezwa na maabara hiyo, na pia Balozi Sefue alikubali ombi la wataalam hao kuwa Balozi Maalum wa Mpango wa Kupunguza vifo kwa akina mama wajawazito na watoto ambao umebuniwa na kupangiwa mkakati katika maabara hiyo.