Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

Katibu Mkuu Kiongozi atembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukagua utekelezwaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu uboreshaji wa huduma za afya hopitalini hapo.


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 23 Novemba, 2015 amefanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukagua utekelezwaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu uboreshaji wa huduma za afya hopitalini hapo ikiwemo agizo la kutaka wagonjwa wasilale chini.

Katika kutekeleza agizo hilo, Balozi Sefue ametembelea wodi mbalimbali katika hospitali hiyo na Taasisi ya Mifupa ya MOI na kushuhudia vitanda 300 na magodoro yake vikiwa tayari vimewekwa wodini na wagonjwa sasa wanatumia hivyo vitanda na hawalali chini kama ilivyokuwa hapo awali. Mbali na vitanda na magodoro hayo zimenunuliwa pia vitanda maalum vya kubebea wagonjwa 30, mashuka 1695 na mablanketi 400. Pesa zilizotumika kununua vifaa hivi zilitokana na maelekezo aliyotoa Mhe. Rais kutaka sehemu ya michango iliyotolewa na wadau mbalimbali kugharimia sherehe za uzinduzi wa Bunge kuelekezwa katika ununuzi wa vitanda na vifaa vingine vya tiba katika hospitali ya Muhimbili.

Akiwa hospitalini hapo, Balozi Sefue alikagua matengezo yanayoendelea ya mashine za MRI na CT-Scan na kutoa siku tatu (3) utengenezaji wa mashine hizo uwe umekamilika na mashine hizo zianze kutoa huduma.

Katibu Mkuu Kiongozi aliagiza pia kuwekwa kwa mfumo maalum wa kielektroniki kubaini madawa yote ya Serikali yanayotolewa na Bohari ya Madawa (MSD),  kuanzia usafirishaji wake hadi hapo zinapotolewa na Daktari kwa mgonjwa. Aidha aliiagiza MSD kufungua maduka ya dawa katika kila hospitali nchini ili kukabiliana na upungufu wa dawa. Hatua hii itaaanza kwa hospitali za rufaa, na kwa hospitali ya Muhimbili itaanza juma lijalo.

Balozi Sefue alitoa wito kwa maduka binafsi ya madawa kuacha mara moja kuuza dawa za Serikali na kueleza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa atakayepatikana anafanya hivyo.

Katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Kiongozi alitumia fursa hiyo kuujulisha umma kuwa Mhe. Rais Magufuli amezuia kufanyika kwa sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka huu na kuamuru siku hiyo itumike kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. Aalieleza kuwa fedha zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya sherehe hizo zitapangiwa matumizi mengine ya kijamii.

Balozi Sefue pia alitumia nafasi hiyo kuendelea kuhimiza watumishi wote wa umma kutimiza ipasavyo wajibu wao wa kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa dhamana walizopewa.  Alipiga marufuku matumizi mabaya ya vifaa vya umma vikiwemo ofisi na vifaa vya Tehama kwa matumizi binafsi ya watumishi wa umma na kuelekeza kila mtumishi wa umma kuvaa kitambulisho chenye jina lake na kufanya kazi kwa uwazi, uadilifu na uaminifu.