Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI ASHIRIKI MKUTANO WA PILI WA JUKWAA LA UONGOZI WA AFRIKA (2ND AFRICAN LEADERSHIP FORUM 2015), DAR ES SALAAM, 30 JULAI, 2015


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 30 Julai, 2015 amekuwa miongoni mwa washiriki wapatao mia moja (100) wa Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Uongozi Afrika uliofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ni mwendelezo wa mfululizo wa Mikutano ya Jukwaa hilo ambalo linaundwa na Marais wa Afrika Wastaafu. Mkutano huo ulifunguliwa na Mwenyeji, Rais (Mstaafu) Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye alielezea furaha yake kuona mwitikio mzuri wa Marais Wastaafu wenzake ambao ni Mhe. Jenerali (Mstaafu) Olesegun Obasanjo wa Nigeria, Mhe. Festus Mogae wa Botswana, Mhe Bakili Muluzi wa Malawi, Mhe Jerry Rawlings wa Ghana na Mhe. Hifikepunye Pohamba wa Namibia.

Aidha, Mhe Dkt. Salim Ahmed Salim, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU) alialikwa kama mzungumzaji.

Mkutano ulipata fursa ya kusikiliza Hotuba ya Msingi (Keynote Address) iliyowasilishwa  kwa umahiri na ufasaha mkubwa na Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, kuhusu Mtangamano wa Afrika (Fursa, Changamoto na Mwelekeo).

Jukwaa la Uongozi la Afrika ni wazo lililobuniw na Mhe Benjamin William Mkapa akilenga kuwakutanisha viongozi wastaafu wa Bara la Afrika katika kutafakari kwa pamoja mustakabali wa Bara hili linalohitaji Ustawi na Ulinzi na Usalama wa watu wake. Mkutano wa kwanza ulifanyika hapa Nchini tarehe 31 Julai, 2014.

Aidha, Taasisi ya UONGOZI ndiyo inayoratibu mikutano hii.