Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI ASHIRIKI MAZISHI YA BIBI MONICA D. LUVANDA


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, leo tarehe 22 Septemba, 2014, ameshiriki mazishi ya aliyekuwa mke wa msaidizi wake Bw. Baraka Luvanda, Bibi Monica D. Luvanda.

 

Marehemu alikuwa mke wa Bw. Baraka Luvanda ambaye ni Mratibu katika Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, alifariki tarehe 19 Septemba, 2014 katika hospitali ya Boshi iliyopo Mbezi kwa Msuguri na kuzikwa katika makaburi ya Agape yaliyopo jirani na Kanisa la Kilutheri Usharika wa Mbezi Luisi.

 

Pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, viongozi wengine wa Serikali walioshiriki mazishi hayo ni Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa Bw. John Haule, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Bw. Jumanne A. Sagini na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Profesa Elisante Gabriel.

 

Pamoja na kuwafariji wafiwa, Balozi Sefue, alieleza kushtushwa kwake na taarifa ya kifo cha ghafla cha mwenza wa mmoja wa Wasaidizi wake ambacho kilitokea wakati yeye pamoja na watendaji wake wakiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro. "Taarifa za msiba huu mzito zilitushtua sote kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa tulikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro ambapo ndipo tulipopata taarifa za  mwenzetu kupata msiba mzito kama huu, mwenyezi mungu awape faraja wafiwa nasi hatuna budi kuwatia moyo katika kipindi hiki kigumu", alisema.

 

Ibada ya mazishi ilifanyika katika kanisa la Kilutheri Usharika wa Mbezi Luisi na maziko yalifanyika katika makaburi ya Agape jirani na Usharika huo, viongozi hao walishiriki katika hatua zote za mazishi hayo.

 

Bwana ametoa na bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe , Ameni.