Habari
Katibu Mkuu Kiongozi ashiriki katika kipindi cha Tunatekeleza TBC - 06 Februari, 2017
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi.,
Mhandisi John H. W. Kijazi leo tarehe 06 Februari, 2017 ameshiriki katika
kipindi cha Televisheni cha TUNATEKELEZA kilichoandaliwa na Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari Maelezo na kurushwa mubashara
kwa takriban dakika 45 na kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC).
Katika kipindi hicho, kilichoongozwa
na Bw. Rashid Salim wa TBC, Katibu Mkuu Kiongozi alielezea kwa ufupi, majukumu anayoyatekeleza
akiwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Mshauri wa Rais wa masuala yote yanayohusu
nidhamu na utendaji Serikalini na Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Katibu Mkuu Kiongozi, alizungumzia
pia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali
ya Awamu ya Tano katika kuimarisha utendaji kazi serikalini, kusimamia nidhamu,
uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma. Aidha, alifafanua
kuhusu zoezi la uhakiki wa vyeti vya Kidato cha Nne (4), Kidato cha Sita (6) na
ualimu vya watumishi wa umma linaloendelea hadi kufikia mwishoni mwa mwezi
Februari, 2017.
Suala lingine alilolizungumzia ni
kuhusu hatua za Serikali ya Awamu ya Tano la kudhibiti matumizi ya fedha za
umma, ambapo alitoa mifano mbalimbali ikiwemo kuhusu fedha zilizookolewa baada
ya kuhairishwa kwa sherehe za maadhimisho ya sikukuu za kitaifa na nyinginezo.
Katibu Mkuu Kiongozi alibainisha kuwa badala ya matumizi hayo, fedha hizo
zilielekezwa katika kufanikisha miradi ya kipaumbele na kutatua kero za
wananchi.
Sambamba na hayo Katibu Mkuu
Kiongozi alizungumzia pia hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano
katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato wenye lengo la kuiwezesha Serikali
kujitegemea na kufanikisha miradi yake, ikiwemo ya kimkakati kwa fedha za
ndani. Vilevile, alizungumzia hatua zilizolenga kupunguza urasimu na kuongeza
ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na sekta binafsi ambayo ni mhimili
muhimu kwa uchumi wa taifa.
Katibu Mkuu Kiongozi alizungumzia
pia jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza uchumi wa nchi, ikiwa
ni pamoja na kuimarisha sekta za kimkakati kama vile viwanda, ujenzi, uchukuzi,
mawasiliano, kilimo, elimu, afya, nishati, maji n.k. Kuhusu sekta ya uchukuzi, alizungumzia
utatuzi wa kero katika utolewaji huduma katika bandari ya Dar es Salaam na uimarishaji
wa sekta ya usafiri wa anga nchini, ambapo mabadiliko makubwa yamefanyika
katika uongozi wa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) na Serikali inatekeleza
mpango kapambe wa kununua ndege mpya kwa ajili ya Shirika hilo ili iweze
kuchangia zaidi kwenye uchumi wa taifa na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, alizungumzia utatuzi wa kero zilizokuwepo kuhusu vituo vya ukaguzi wa
magari ya mizigo yanayokwenda nje ya nchi kutokea bandarini, ambapo vituo vya
ukaguzi vimepunguzwa kufikia vitatu (3) kwa Ukanda wa Kati na vinne (4) kwa
Ukanda wa Dar es Salaam. Kuhusu viwanda alitoa mifano michache ya viwanda
vikubwa vilivyojengwa na vinavyokusudiwa kujengwa, vitakavyowezesha kutimia kwa
dhima ya uchumi wa viwanda.
Katibu Mkuu Kiongozi aliongelea
masuala mengine muhimu ikiwa ni pamoja na mchakato wa Serikali kuhamia Dodoma,
ambapo aliweka bayana kuwa baadhi Wizara zimeshaanza kuhamia katika Makao Makuu
ya Serikali, na nyingine zitatekeleza suala hilo kwa awamu bila kuathiri
utendaji kazi Serikalini. Hali kadhalika, Katibu Mkuu Kiongozi alizungumzia na
kufafanua kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo kwa kipindi cha
Miaka Mitano kuanzia 2016/17 hadi 2020/21 na Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi
kufikia mwaka 2025.
Mwishoni mwa kipindi hicho, Katibu
Mkuu Kiongozi alitoa wito kwa Wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi
zinazofanywa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli na Serikali yake katika kutekeleza ahadi, mikakati na mipango
mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wote.
Kabla ya kushiriki
kwenye kipindi hicho, Katibu Mkuu Kiongozi alikutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji
Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba kuhusu mustakabali na maono ya Shirika hilo.