Habari
KATIBU MKUU KIONGOZI, AONGOZA WATUMISHI WA UMMA KUMUAGA RASMI MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA. 22 OKTOBA, 2015, UKUMBI WA MLIMANI CITY, DAR ES SALAAM.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 22 Oktoba, 2015 ameongoza Watumishi wa Umma kumuaga rasmi Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeelekea kumaliza kipindi cha uongozi wake.
Katika hafla hiyo, Balozi Sefue ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi wa Umma alimpongeza Rais Kikwete kwa kuwezesha kupatikana kwa mageuzi na mafanikio makubwa ya Utumishi wa Umma katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake. Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kazi, kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kuimarishwa kwa mifumo ya wazi ya ajira, upandishwaji vyeo na majadiliano kupitia mabaraza ya wafanyakazi.
Aidha Katibu Mkuu Kiongozi alimshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi wa Serikali yake kuanzisha na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa Serikali, kuanzisha mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) yenye kufuatilia utekelezaji na tathmini Serikalini na kuanzishwa kwa Watumishi Housing Company yenye lengo la kuboresha makazi ya Watumishi wa umma hasa wastaafu. Kwa mujibu wa Balozi Sefue, mifumo hii iliyoasisiwa na kusimamiwa na Rais Kikwete imeboresha na kubadilisha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi Serikalini.
Balozi Sefue alihitimisha hotuba yake kwa kumtakia Rais Kikwete na familia yake maisha marefu yenye afya njema na furaha tele.
Awali, akisoma Risala ya watumishi wa umma, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watumishi wa Umma ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. HAB Mkwizu kwa niaba ya watumishi alimshukuru Rais Kikwete kwa juhudi kubwa alizofanya kuboresha utendaji kazi katika utumishi wa umma na kuboresha mara kwa mara maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo mishahara, huduma za Mifuko ya Hifadhi ya jamii, mafao ya wastaafu na Bima ya Afya.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Serikali, Watendaji Wakuu wa Mahakama na Bunge, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika na Wakala za Serikali, Wenyeviti wa Bodi za Taasisi za Umma, Makatibu Tawala wa Mikoa na Viongozi wa Mabaraza ya Wafanyakazi.
Wakati wa sherehe hizo, Mhe. Rais alipokea zawadi kadhaa kutoka kwa watumishi wa Umma kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuleta mageuzi na mafanikio ya utumishi wa umma. Aidha Mhe. Rais alitumia fursa hiyo kuhimiza watumishi wa umma kuimarisha utendaji kazi wao na kuachana na ukiritimba unaodhoofisha huduma wanazozitoa kwa jamii. Pia aliwashukuru watumishi umma kwa zawadi na ushirikiano mzuri waliompa wakati wa uongozi wake.
NB: Soma hotuba ya katibu Mkuu Kiongozi katika tovuti hii