Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi

Habari

KATIBU MKUU KIONGOZI AONGOZA MKUTANO WA FARAGHA (RETREAT) WA MAKATIBU WAKUU NA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA DODOMA TAREHE 27 OKTOBA, 2014


Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue leo tarehe 27 Oktoba, 2014 amefungua rasmi Mkutano wa Faragha (Retreat) wa Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha St. Gaspar, Dodoma.

 

            Mkutano huo ni wa siku mbili, ambapo washiriki watapata fursa ya kukumbushana masuala mbalimbali yanayohusu mifumo ya Ufuatiliaji, Tathmini na Udhibiti wa matumizi ya rasilimali za Serikali.

 

            Kabla ya ufunguzi wa Mkutano, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi alipata fursa ya kuwasalimia washiriki wa mkutano ambapo aliwakaribisha Dodoma na kusema kuwa, ilikuwa sahihi kuchagua Dodoma kuwa Mwenyeji wa mkutano huu muhimu kwani Dodoma ni Makao Makuu ya nchi. Mheshimiwa Nchimbi aliwasihi washiriki kutafakari kwa pamoja dhana na nadharia ya mazingira yanayowazunguka ili wamsaidie vizuri Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania.

 

            Katika hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue amehimiza sana suala la Ufuatiliaji na Tathmini, akasema yapo baadhi ya maeneo ndani ya Utumishi wa umma ambako wamejitahidi kuanzisha na kutekeleza mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini lakini sehemu kubwa wanaikwepa mifumo hiyo kwa kuwa inawabana na akaahidi kuwa watumishi wa aina hiyo watashughulikiwa.

 

            Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi ameeleza kusikitishwa kwake kwa tabia ya wizi wa mali ya umma kutokana na udhibiti hafifu na akahimiza kuwa tabia hiyo ikome na kwamba watakaobainika kuendelea na tabia hiyo watakumbana na hatua za kisheria.

 

            Mkutano wa Faragha wa Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa ni utaratibu aliouanzisha Katibu Mkuu Kiongozi mwaka jana (2013) wa kuwakutanisha Viongozi Waandamizi wa Serikali kubadilishana uzoefu, maarifa na ujuzi katika hali ya uhuru, uwazi na ukaribu miongoni mwao, bila kukwazwa na taratibu za Kiitifaki. Mkutano huu ni wa pili kufanyika, ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika mwezi Septemba 2013.