Habari
Katibu Mkuu Kiongozi amuwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya 15 ya siku ya Wahandisi Tanzania, Dodoma, 7 Septemba, 2017
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mha. John W.H. Kijazi, leo tarehe 7 Septemba, 2017 amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika ufunguzi wa Maadhimisho ya 15 ya Siku ya Wahandisi Tanzania yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Dkt. Jakaya Kikwete, mjini Dodoma kwa muda wa siku mbili, tarehe 7 -8 Septemba, 2017.
Maadhimisho hayo
yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (Engineers Registration
Board) na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yana mada kuu isemayo “Jukumu la Sayansi,
Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika kukuza Viwanda kwa Maendeleo ya Kijamii
na Kiuchumi.”
Katika siku mbili za
Mkutano huo, Wahandisi wapatao takriban 2,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini
wanajadili masuala mbalimbali kuhusu taaluma ya Uhandisi zikiwemo changamato na
fursa za Wahandisi katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21). Aidha, watashiriki katika maonesho ya
kiufundi na kibiashara yanayoonesha bidhaa zinazotokana na ubunifu wa kihandisi.
Katika hotuba yake
ya ufunguzi, Katibu Mkuu Kiongozi aliishukuru Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Bodi ya Usajili wa Wahandisi Mawasiliano kwa mwaliko wa kuhudhuria maadhimisho
hayo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza Mjini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi na
Serikali. Aidha, aliipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa
kuandaa maadhimisho hayo na kuchagua mada kuu inayoakisi azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuzipatia ufumbuzi changamoto za
msingi za Watanzania, hususan walio maskini.
Katibu Mkuu Kiongozi
alisisitiza kuwa Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani inategemea
Wanasayansi kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali za
kimaendeleo. Aidha, alikiri kuwa Serikali inafahamu kuhusu idadi isiyokidhi ya
Wahandisi na kutaja hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili kuongeza idadi hiyo
ikiwa ni pamoja na kuboresha elimu ya sekondari na kuhamasisha vijana wasome
masomo ya sayansi; kuongeza nafasi za masomo ya Uhandisi katika Vyuo vikuu; na
kuongeza idadi ya Wasichana wanaosoma Uhandisi katika vyuo vikuu na vyuo vya
mafunzo ya ufundi.
Kuhusu ushiriki wa
Wahandisi wa ndani katika utekelezaji wa miradi ya ndani, Katibu Mkuu Kiongozi
alisisita umuhimu wa utayari na uwezo wao ambavyo ndio vitakaowawezesha kuwania
fursa zilizopo na zitakazokuwepo na kuhimili ushindani katika tasnia hiyo.
Katika suala la kuwajengea utayari na uwezo Wahandisi wa ndani, Katibu Mkuu
Kiongozi aliishukuru Bodi ya Usajili wa Wahandisi na wadau wengine, ukiwemo
Ubalozi wa Norway unafadhili mafunzo kwa vitendo kwa Wahandisi Wahitimu
wanawake na Benki ya Dunia inayofadhili mafunzo hayo kupitia mradi wa “Dar es
Salaam Urban Transport Improvement Project.”
Katika hotuba hiyo
pia, Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Sekta ya
Umma na Binafsi na miongoni mwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. “Hivyo,
rai yangu kubwa kwenu ni kwa wadau wote kutoka Sekta Binafsi na ya Umma
kudumisha ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa Tanzania ya Viwanda”
alisema.
Akiongea kwa niaba
ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mheshimiwa Simon Odunga
aliwakaribisha Wahandisi Mjini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi na Serikali. Aidha,
aliwafahamisha kuwa Dodoma inazo fursa mbalimbali kwa Wahandisi kufuatia uamuzi
wa Serikali wa kuhamia Dodoma.
Naye Mwenyekiti wa
Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mha. Prof. Ninatubu Lema alimshukuru sana Katibu
Mkuu Kiongozi kwa kukubali mwaliko wa Bodi na kuelezea furaha waliyokuwa nayo
Wahandisi kwa kuwa naye katika Maadhimisho hayo, kuzingatia taaluma yake ya
Uhandisi. Aidha, alieleza azma ya
Wahandisi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda nchini
Tanzania na kutatua changamoto zinazowakabili Wahandisi. Vilevile aliiomba
Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi kuruhusu miradi mikubwa ya ujenzi wa
miundombinu ya reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari na mabomba ya
usafirishaji wa mafuta na gesi asilia itumike kama madarasa kwa Wahandisi
vijana; iweke utaratibu mzuri wa kuwajengea uwezo Wahandisi wa ndani kwa
kutoruhusu kampuni za kandarasi kutoka nchi za nje kutofanya kazi nchini bila
ya ubia na makampuni ya ndani; na ipige marufuku uingizwaji wa vifaa vya ujenzi
ambavyo vinazalishwa na viwanda vya ndani.
Katibu Mkuu Kiongozi alipokea maombi hayo na kuhaidi kuwa Serikali itayafanyia kazi pindi yatakapowasilishwa rasmi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi.