Habari
Katibu Mkuu Kiongozi ameongoza Mkutano wa Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Vikao vya Kazi vya Makatibu Wakuu wa Wizara zote hapa Dodoma 01 Machi, 2017.

Katibu Mkuu Kiongozi ameongoza Mkutano wa
Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Vikao vya Kazi vya Makatibu Wakuu wa Wizara
zote hapa Dodoma 01 Machi, 2017.
Leo tarehe 1 Machi,
2017 Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, Balozi Mha. John W. H. Kijazi ameongoza
Mkutano wa Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Vikao vya Kazi vya Makatibu Wakuu
wa Wizara zote hapa Dodoma.
Hii ni mara ya
Kwanza kwa Mkutano na Vikao hivyo kufanyika mjini Dodoma tangu Serikali ya
Awamu ya Tano ifanye uamuzi wa kuhamia Dodoma.
Vikao hivyo vitakavyodumu
kwa siku tatu (3) vitapokea na kujadili agenda mbalimbali zitakazowasilishwa na
Wizara, zinazohusu masuala ya takwimu; ujenzi wa miundombinu; miradi mikubwa ya
kimkakati ikiwemo ya sekta ya mafuta na gesi; mazingira ya uwekezaji na
biashara na namna ya kukabiliana na changamoto zake.
Kamati Maalum ya
Makatibu Wakuu ndicho chombo Kikuu cha Kitaalam chenye jukumu la kupokea,
kuchambua na kujadili nyaraka mbalimbali zinazowasilishwa na Wizara kabla hazifikishwa
kwenye Baraza la Mawaziri kwa mijadala na maamuzi.
Tangu Serikali ya
Awamu ya Tano iingie madarakani, Baraza la Mawaziri limeshakutana mara 13 na
kufanya maamuzi makubwa na muhimu kwa mustakabali wa Tanzania na Watanzania,
ukiwemo uamuzi muhimu kuhusu ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini
Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Katika mazungumzo
yao yaliyofanyika tarehe 25 Februari, 2017, Marais wa Uganda na Tanzania
walielezea dhamira yao ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa bila ya kuchelewa.
Mkutano wa Kamati
Maalum wa Makatibu Wakuu wa Wizara zote ni kielelezo dhahiri cha utekelezaji
kwa vitendo azma ya Serikali kuhamia Dodoma. Hadi kufikia tarehe 1 Machi, 2017
takriban Wizara zote za Serikali zilikuwa zimeshahamia Dodoma. Zoezi hili
muhimu lilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim M. Majaliwa (MB) mnamo
tarehe 30 Septemba, 2016.
Ofisi ya Katibu
Mkuu Kiongozi inawashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kuunga mkono jitihada
mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Tano zenye lengo la kujenga Tanzania mpya
yenye maendeleo zaidi kwa watu wote na uchumi imara unaotegemea Viwanda.
Aidha, inatoa rai
kwa wananchi na watu wote kuzitumia kikamilifu fursa mbalimbali zilizopo katika
Mji Mkuu wa Tanzania na Makao Makuu ya Serikali –Dodoma, ambazo zimehuishwa
kufuatia uamuzi huu muhimu wa Serikali. Fursa hizo ni pamoja na biashara na uwekezaji;
na huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii. PAMOJA TUJENGE TANZANIA MPYA.
Imetolewa na Ofisi
ya Katibu Mkuu Kiongozi
01/03/2017
DODOMA